Na Edigar Nkilabo,
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imevijumuisha vijiji 16 kati ya 71 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi utakaowawezesha wananchi kushiriki kupanga matumizi ya ardhi yao ili waweze kuitumia ardhi hiyo kwa tija katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na kuinua hali zao za maisha.
Hayo yamesemwa Wilayani Sikonge na Afisa Ardhi Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi(NLUPC), Nyirembe Munasa ambapo amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa ilani ya CCM inayosisitiza kuwapa wananchi haki ya umiliki wa ardhi ambao utawawezesha kupata hati za kimila na kufanya shughuli zao za maendeleo kwa tija.
“Eneo kubwa la Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ni misitu na hifadhi ni eneo dogo la ardhi ambalo wananchi wanatumia kwa makazi hivyo nyenzo pekee ni kuandaa mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi ili wananchi wapate maeneo kwa ajili ya kilimo cha tumbaku,uwindaji, maeneo ya huduma za jamii na makazi.Pia wananchi watapata hati za kimila ambazo zitawawezesha kukopa na kupata mitaji ya kufungua biashara na kujikwamua kiuchumi”amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Cornel Lucas Magembe amesema programu hiyo ni jawabu la changamoto za wakazi wa Sikonge ambao wamekuwa wakikabiliwa na migogoro ya ardhi kutoka na mwigingiliano wa shughuli za kibinadamu.
“Kesi nyingi tunazotatua za migogoro ya ardhi viongozi zinatokana na kukosekana kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi hivyo unakuta eneo la makazi hapo hapo kuna nyumba za ibada, maeneo ya masoko hayaeleweki naamini programu hii imekuja muda muafaka kwani migogoro itapungua kwa kiasi kikubwa kwakweli tunamshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka Sikonge kupitia mradi huu unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi”amesema.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Kabanga ambao ni miongoni mwa wanufaika wa programu hii wamesema elimu waliyopatiwa katika mpango ambao ni shirikishi imewafumbua macho hivyo migogoro ya kugombea mipaka baina ya kijiji na kijiji haitatokea tena na kila mwananchi atapata haki ya kumiliki kipande chake cha ardhi kwa mujibu wa sheria.
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inatarajia kutekeleza zoezi hilo katika Halmashauri 21 zilizopo kwenye mikoa 14 kupitia programu ya upangaji matumizi ya ardhi katika vijiji 333 vilivyoandaliwa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa