Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kanda ya Magharibi imetangaza kumalizika kwa mafunzo ya siku saba kwa wajumbe wa bodi na wawakilishi wa vyama vya ushirika vya msingi wilaya ya Sikonge. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima, ili kufikia malengo ya uzalishaji bora wa zao la tumbaku.
Mafunzo hayo yamejumuisha nyanja mbalimbali muhimu za ushirika, zikiwemo masuala ya rushwa katika vyama vya ushirika, elimu ya uhamiaji kwa wanaushirika, maadili ya viongozi, na mikataba ya kazi kwa watendaji wa vyama vya ushirika. Wajumbe walipata pia fursa ya kula kiapo cha uadilifu cha viongozi wa vyama vya ushirika wilayani Sikonge, kilichoongozwa na mwanasheria kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mgeni rasmi katika kuhitimisha mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Juma Nkumba, amewaonya viongozi wa vyama vya ushirika kuacha tabia ya "uungu mtu" ili waweze kuwatumikia wanachama kwa haki na ufanisi. Alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kuwa waadilifu, kuwa na maadili ya uongozi, na kuwa viongozi wanaopatikana kirahisi kwa wanachama wao.
Aidha, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Bw. Venace Msafiri, amewasihi wajumbe wa vyama vya ushirika kujiunga na bima ya kilimo. Amesema kuwa bima hiyo itawawezesha kulinda mitaji yao na shughuli zao za kilimo, hasa wakati wa majanga kama uhaba wa mvua au dhoruba, ambapo fidia inaweza kutolewa kwa uharibifu wa mazao yao.
Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Lucas Magembe, amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa SACCOs za wakulima wa tumbaku. Amesema kuwa SACCOs hizi zitasaidia wakulima kutatua changamoto zao za kifedha, huku wakiepuka vishawishi vya kuuza tumbaku soko huria, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Mkuu huyo ameongeza kuwa SACCOs pia zitakuwa na manufaa kwa wakulima katika kujiandaa na msimu wa kilimo.
Mhe. Magembe ametumia jukwaa hilo kutoa hamasa kwa wakulima kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wenzao kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Wilaya ya Sikonge imekuwa ya kwanza kunufaika na mafunzo haya, ambapo zaidi ya wanachama 400 wa vyama vya ushirika kutoka mkoa wa Tabora wamepata elimu na ujuzi wa kuboresha shughuli zao za kilimo na ushirika.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa