Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Young Strong Mothers Foundation ya mjini Morogoro imetoa msaada wa vifaa vya michezo kwa shule tatu za sekondari zilizopo wilayani Sikonge ambazo ni Shule ya Sekondari Mkolye,Tutuo na Mole. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na sare za mchezo wa mpira wa miguu kwa shule tatu,mipira,kamba za mazoezi,vifaa vya kufanyia mazoezi uwanjani “cones”,soksi ,leso pamoja na taulo za kike.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Bi. Jackline Bomboma amesema “Sisi kazi yetu kubwa ni kushirikiana na Serikali pamoja na wazazi na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni,ndoa za utotoni na kusitisha masomo kwa watoto wa kike shuleni,na tunafanya hivyo kuwasaidia vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya shule kama vile viatu soksi,sketi,shati,begi,madaftari,taulo za kike,mafaili ya kutunzia mitihani,lakini pia nakuendelea kutoa elimu za wao waweze kujitambua,kujithamini na kujituma katika elimu”.
Zoezi hilo limeshuhudiwa na,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na diwani wa kata ya Tutuo Mhe. Rashid Magope, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Bw. Charles Mwita kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge,diwani wa kata ya Mkolye, Mhe. Omar Kategile na diwani kata ya Mole,Mhe. Seif Mahanga pamoja na wakuu wa shule za sekondari Tutuo,Mkolye na Mole.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa leo hasa kwa kuchagua Sikonge badala ya maeneo mengine,lakini pia amewasihi watoto wa kike kuzingatia masomo na kuepuka kulubuniwa na watu waovu “hususani ninyi wasichana,mmekuwa mkidanganywa ,mkilubuniwa na kuachia njiani masomo yenu,lakini kupitia taasisi hii yako mambo mtasaidiwa”amesema Mhe. Magope.
Muasisi wa taasisi ya Young Strong Mothers Foundation Bi.Jackline Bomboma ni mzaliwa wa Sikonge katika kijiji cha Kikungu,amepata ushawishi wa kuja kufanya kazi Sikonge baada ya kukutana na Mbunge wa jimbo la Sikonge Mhe. George Joseph Kakunda na alimuahidi kuwa wakati muafaka ukifika atakuja Sikonge.Tangu aanze kufanya kazi Sikonge amefanyika kuwa msaada mkubwa sana katika sekta ya elimu hasa katika kusaidia watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa