Mkutano mkuu wa wakulima wa tumbaku wa chama cha msingi SULUHU uliofanyika leo, Agosti 31, 2024, wilayani Sikonge, katika kijiji cha Chang'ombe kata ya Mkolye kimepata umaarufu na kupongezwa kwa mafanikio yake makubwa mwaka huu. Mkutano huu, uliojaa hisia za furaha na matumaini, uliwashirikisha wakulima, viongozi wa AMCOS, na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Tabora Ndg. Venance Msafiri,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo wa mwaka.
Katika mkutano huo, chama cha SULUHU kimepata wasaa wa kusoma mapato na matumizi ya fedha zake, huku wakionesha uwazi wa hali ya juu katika usimamizi wa rasilimali. Hali hii ilipokelewa vizuri na wajumbe wa mkutano, ambao walithibitisha utendaji mzuri wa chama hicho katika kuendesha shughuli zake. Mrajisi Msaidizi alitoa ahadi muhimu kwa chama hicho, akisema kuwa atahakikisha usajili wa kudumu unapatikana mapema, jambo ambalo litazidi kuimarisha na kuthibitisha uwepo wa chama hicho katika mfumo wa kilimo cha tumbaku.
Katika tathmini ya mwaka huu, imebainika kuwa chama cha SULUHU kimefanikiwa kulipa wakulima kwa asilimia 92.5 ya malipo yao.Ikiwa ni kiwango kikubwa cha kuridhisha, ikilinganishwa na viwango vya kawaida vya kulipa. Mafanikio haya yameongeza matumaini kwa wakulima na kuimarisha imani yao katika usimamizi wa chama chao.
Hata hivyo, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Tabora Ndg. Venance Msafiri hakukosa kutoa kauli kali kuhusu suala la utoroshaji wa tumbaku.Amekemea tabia hii ambayo imekuwa ikikumba sekta ya kilimo cha tumbaku nchini, akisema kuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya chama na ustawi wa wakulima. Amewaaasa viongozi wa AMCOS na wakulima kuhakikisha kwamba tabia hiyo inakomeshwa ili kuweza kupata faida kamili kutokana na kilimo cha tumbaku na kufikia malengo ya maendeleo ya kilimo katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine amewapongeza kwa dhati viongozi wa Amcos kwa kutekeleza kwa haraka wazo la uanzishwaji wa Saccos ikiwa ni hatua muhimu sana katika kupambana na hali duni ya uchumi wa wakulima wa tumbaku kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu itakayoimarisha uchumi wa wakulima hao.
Kwa ujumla, mkutano huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa chama cha SULUHU, ukiashiria mwanzo mpya wa matumaini na maendeleo katika kilimo cha tumbaku wilayani Sikonge. Wakulima wameonesha kuridhika na usimamizi bora wa chama chao, huku viongozi wakiahidi kuendelea kuboresha huduma na kupambana na changamoto zilizopo.
USHIRIKA! PAMOJA TUJENGE UCHUMI.
“Serikali za Mitaa,Sauti ya Wananchi,Jitokeze kushiriki Uchaguzi.”
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa