SIKONGE YAZINDUA MNADA MKUBWA WA MIFUGO.
Halmashauri ya Sikonge yazindua Mnada mkubwa wa Mifugo na bidhaa katika kata ya Mpombwe uliojengwa kwa mapato ya ndani.
Mnada huo uliozinduliwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya alisema kuwa mnada huo ni mkubwa ukilinganishwa na ya minada mitano iliyopo katika halmashauri ya Sikonge, ambao umetumia gharama za Tsh. Mil 29 hadi kukamilika kwake.
Aliongeza kuwa hiyo ni fursa pekee kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kwani utaondoa adha ya kupeleka mifugo yao mbali ambapo wafugajia walikuwa wakipeleka mifugo kwenye Wilaya nyingine jambo lililokuwa linapelekea changamoto ya kutembea umbali mrefu vilevile kupoteza mapato ya Halmashauri. Hivyo alishauri wafugaji kuitumia fursa hiyo vizuri.
Akitoa takwimu za Mifugo inayotegemewa kuuzwa kwenye mnada huo. Kaimu mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Mipawa Majebele alisema kuwa mnada huo unategemewa kuuzwa ng’ombe zaidi ya mia nane (800) na mbuzi zaidi ya mia nne (400) jambo ambalo litaipatia Halmashauri mapato, na zaidi ya Mil. 2 zinategemewa kukusanywa Kwa mwezi.
Mwemyekiti wa Halmashauri Mhe. peter Nzalalila akizungumza na wafugaji (hawapo pichani) siku ya Uzinduzi wa Mnada.
Aidha aliwataka wafugaji kuitunza mifugo yao kwa kufuata njia za kitaalamu kwa kuitibu na kuiosha kwenye majosho ambayo tayari yamefufuliwa ili kuipa mifugo thamani katika soko la mifugo huku akitaja ugonjwa wa mapele ngozi ambao umekuwa tishio kwa mifugo kuwa unatibiwa na kuwataka wafugaji wasisite kupata ushauri toka kwa maafisa mifugo mara watakapoona dalili kwenye mifugo yao sanjari na kuchanja chanjo ya mifugo mara kwa mara kulingana na utaratibu uliowekwa na wataalam.
Akigusia changamoto ya njia za kupitishia Mifugo Majebele alisema kuwa vijiji vinaweza kutatua changamoto hiyo kwa kutenga mita 70 kwa ajili ya kuruhusu mifugo hiyo kupita na njia hizo ziheshimiwe kwani hawako tayari kuona mifugo ikipata tabu tena.
Uzinduzi wa mnada huo ulipokelewa kwa shangwe kubwa na wafugaji wakiwakilishwa na Diwani wa kata ya Mpombwe Mhe. Juma Mdulla aliyetoa shukrani zake kwa serikari huku akisema kwa niaba ya wanampombwe wanaipongeza Serikali kupitia Halmashauri kwani wameweka jambo la kihistoria ambalo litakumbukwa. Wanaahidi kuitumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi hivyo wanawakaribisha wafugaji na wafanyabiashara mbalimbali kufika Mpombwe kwa ajili ya kufanya biashara.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA TEKINOLOJIA HABARI NA MAWASILIANO(TEHAMA)
SIKONGE
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa