Na, Linah Rwambali
WIZARA ya Katiba na sheria imetoa mafunzo ya uraia na utawala bora kwa viongozi 41 wa mamlaka za serikali za mitaa katika Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Wakili wa serikali toka wizara ya Katiba na sheria Dorice Dario alieleza malengo ya kutolewa kwa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo viongozi wa Mamlaka za usimamizi wa serikali za Mitaa,wataalamu katika Halmashauri na viongozi wa serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwajengea uwezo kuhusu haki na wajibu, Demokrasia na Utawala Bora, madaraka kwa umma,ulinzi na usalama, kukuza na kuendeleza uzalendo na utaifa miongoni mwa watumishi wa umma na mengineyo” alisema.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Katibu Tawala wa Wilaya ya Sikonge Andrea Ng’hwani aliishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa mafunzo hayo na kuwaagiza watendaji na wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kufanyia kazi waliyojifunza.
“Mada zote zilozofundishwa msingi wake mkubwa ni kuleta amani na utulivu katika jamii yetu hivyo naomba watendaji mkazingatie hayo yote ili kudumisha amani katika maeneo yenu mnayoongoza” alisema.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mole Emmanuel James alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa mwongozo wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama viongozi.
“Elimu ya utawala bora tuliyoipata leo imetukumbusha kuwajibika vyema katika vituo vyetu vya kazi na kutujengea weledi katika majukumu yetu” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa