SIKONGE YAFUNIKA UZINDUZI WA SEMA USIKIKE
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imezindua rasmi Kampeni ya SEMA USIKIKE dhidi ya Rushwa, Mimba na Ndoa za Utotoni katika Viwanja vya TASAF. Uzinduzi huo ambao ni wa Kimkoa umefanyika leo kwa kuwashirikisha wanafunzi wenyewe ambao wamefikisha jumbe mbalimbali kuhusu Rushwa na Mimba za utotoni kupitia Maigizo, Nyimbo, Ngonjera, Ngoma za jadi na Mashahiri.
Mkurugenzi wa Taasisi ya “Creative Plan” yenye kali mbiu ya SEMA USIKIKE, ndugu Juma Mtetwa akasema, “hakika Sikonge mmefunika, katika sehemu zote tulizopita sijaona kama Sikonge.” Aliyasema hayo baada ya kuona jumbe mbalimbali zilizowasilishwa na wanafunzi wenyewe, na akasema hili ndilo lengo kuu la kauli mbiu yao.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Simon Ngatunga alifurahishwa sana na maandalizi waliyoyaonesha wanafunzi katika uzinduzi huo. “Mataifa makubwa duniani yaliyopiga hatua mbalimbali za kimaendeleo, (mfano. Japan) yalianzia katika msingi wa watoto, hivyo mtoto anakua akijua jambo Fulani ni baya kwa Nchi yangu (mfano. Kutolipa kodi ya Nchi)”, alisema Mkurugenzi huyo.
…"Hivyo kwa kuwashirikisha watoto wenyewe katika masuala ya Rushwa, Mimba na Ndoa za utotoni ni kuwajengia msingi imara utakaowafanya watoto hao kuwa imara siku za badae watakapokuwa viongozi.” Aliyasema haya na kisha kumkaribisha Mgeni Rasmi ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Peres Magiri.
Mgeni Rasmi aliwapongeza sana walioandaa zoezi zima la uzinduzi na walioshiriki hasa Mkurugenzi wa “Creative Plan”. Pia aliwaeleza wananchi pamoja na watumishi kuwa Mgeni Rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Mhe. Agrey Mwanri lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake hakuweza kufika hivyo alimuomba amuwakilishe katika hafla hiyo.
Aidha, Mgeni rasmi alisema, “Rushwa ni adui wa haki, hata ninyi mmeyaeleza katika maigizo yenu hapa, hata Rais wa Nchi analikemea na kupambana juu ya hili kila siku na nyote ni mashahidi, hebu tumpigie makofi Mhe. John Magufuli.” Alisisitiza kushirikiana kwa pamoja juu ya kupambana na rushwa kwani TAKUKURU peke yao hawatoweza.
Akizungumzia jambo la Mimba za utotoni alisema, “wanafunzi ngojeni niwafundishe mbinu nyingine ya kuepukana na vishawishi vya mafataki, akikusemesha mjibu kwa lugha ya kizungu kwani waliowengi hawajui lugha hiyo, mwisho wa siku ataishia kusema… anajifanya msomi…, acheni waseme hivyo lakini umeshamuepuka.” Aliendelea kusisitiza kuwa kwa kuwaepuka hao mafataki na watu wa aina hiyo, tutapata Wabunge, Mawaziri na hata Marais.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA TEHAMA
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa