Wilaya ya Sikonge imeadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kufanya zoezi la kupanda miti, lililoendeshwa na Kaimu Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bi. Faraja Hebel.
Katika maadhimisho haya, Bi. Hebel amewaongoza watumishi pamoja na wananchi wa wilaya hiyo katika Shule ya Sekondari Sikonge, ambapo zoezi la upandaji miti ya kivuli limefanyika. Zoezi hili limefanyika kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), na jumla ya miche 1000 ya miti ya kivuli imepandwa katika maeneo mbalimbali ya taasisi za serikali na za binafsi wilayani Sikonge.
Bi. Hebel amesisitiza kuwa maadhimisho haya yana lengo la kuhamasisha wananchi katika uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za taifa. Ameongeza kuwa upandaji miti ni njia moja wapo ya kudumisha usalama wa mazingira,kuleta kivuli kwa wanafunzi hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande mwingine, viongozi wa TFS wilayani Sikonge wameeleza furaha yao kwa kushirikiana na jamii katika kuendeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, huku wakisema kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kuchukua hatua katika kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara inasema, "Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo Yetu," ambayo imejikita katika kuonesha mchango wa wananchi katika maendeleo ya taifa lao.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa