Na Halidi Nyange na Mwatebela Gadi
Mji wa Sikonge ni miongoni mwa miji iliyopo katika maeneo yenye hali ya Kitropiki, hivyo upatikanaji wa maji ya ardhini ni mgumu. Hata hivyo, kulingana na jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imeendelea na kupambana na uhaba wa maji katika mji huo.
Halmashauri hiyo imeweza kuboresha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 5 za upatikanaji wa maji Mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 62 za upatikanaji wa maji Mwaka 2017 katika mji wa Sikonge. Hatua hiyo imefikiwa kwa kujenga Magati na kusambaza mabomba ya maji majumbani kutoka katika chanzo cha maji ya bwawa la Utyatya lililopo umbali wa kilomita 12.6.
Aidha, Mhandisi wa Maji Wilaya, Paschal Ngunda alisema, “hadi kufikia 2025 tunategemea kufikia asilimia 100 za upatikanaji wa maji katika mji wa Sikonge.” Mhandisi huyo alisisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji hasa mabwawa ili viweze kudumu na kuwahudumia wananchi.
Hayo yalisemwa katika kuhitimisha Wiki ya Maji katika Kijiji cha Utyatya Kata ya Kisanga ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri. Wiki hiyo ya maji Duniani yenye Kauli mbiu, Hifadhi Maji na Mfumo wa Ikolojia kwa Manufaa ya Jamii ilianza tarehe 16 Machi na kuhitimishwa 22 Machi 2018.
Katika kuhitimisha wiki ya maji, Mgeni rasmi alikagua upandaji wa miti kandokando ya bwawa la maji Utyatya pamoja na kushiriki upandaji wa miti katika kijiji hicho. Akifunga wiki ya maji Duniani alisema, “shughuli za ujenzi wa makazi na kilimo katika maeneo ya bwawa lolote lililopo Wilaya ya Sikonge, ziondolewe mara moja, wavamizi wakamatwe mara moja na nyumba zivunjwe! sihitaji kutoa siku.”
Aidha, katika kilele cha wiki hiyo mgeni rasmi alizindua Gati moja la Maji Mjini Sikonge na kuwasisitiza wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu ya maji ili upatikanaji wa maji uwe endelevu. Ujenzi wa Gati hilo umegharimu Milioni nne. Wananchi hasa kina mama wamefurahia sana uzinduzi wa gati hilo kwani litarahisisha upatikanaji wa maji na kwa gharama ndogo ya shilingi 50 kwa lita 20, kwani awali walikuwa wakinunua maji kwa shilingi 500 kwa lita 20.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA TEHAMA
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa