SIKONGE IMEWEZAJE?
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Bwa. Simon Ngatunga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, ametoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Milioni 138 kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu katika hafula fupi iliofanyika leo katika Ukumbi wa Mwanambuya.
“Siku hizi tunasema Mwanamke akiweza, anawezesha familia nzima…” hayo yamesemwa na Mkurugenzi Ngatunga ambapo pia alisimulia namna Mama yake alivyokuwa akipambana kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kijasiriamali ili kumsomesha. “…na pengine mama yangu asingefanya vile nisingefika hapa nilipo” alisema Mkurugenzi huyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inapoelekeza fedha kwenye makundi ya wanawake, inajua Taifa limekombolewa kwa kuwa uchumi wa familia, Wilaya na Taifa kwa ujumla unakuwa, na ndio maana Halmashauri inawekeza zaidi kwenye vikundi hivi. Pia alitoa historia ya kuanzia Mwaka jana ambapo Halmashauri ilitoa Milioni 121 kwa vikundi 119 na Mwaka huu imetoa Milioni 138 kwa vikundi 104.
Mkurugenzi Ngatunga aliendelea kusema kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuelekeza asilimia 10 ya fedha za Mapato ya ndani katika makundi matatu, wanawake, vijana na walemavu. Kwa maana ya kuwa fedha iliyokusanywa kutoka kwao inarudi tena kwao kuajili ya kuinua uchumi wao, lakini pia kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa kwa asilimia 100.
Aidha, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Margaret Mussai alisema, “Chama Tawala kinazungumzia Serikali, hakizungumzi mtu mmoja wala hakiangalii kabisa chama Kingine, kwa hiyo lazima mfanye kazi na kuhakikisha kinapata nguvu ya kuwatetea zaidi na zaidi.” Aliyasema hayo kuonesha msisitizo wa namna Serikali yao inavyowajali hasa wananchi wa chini.
Nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sikonge, Bi. Anna Chambala alifurahishwa sana na kumshukuru Mkurugenzi Ngatunga kwa namna ya pekee anavyotekelaza ilani ya Chama Tawala. “Pamoja na mikopo hii mnayokwenda kuipata siku ya leo, niwaombe sana mama zangu, niwaombe sana vijana, kama Serikali ilivyotupa kipaumbele sisi wanawake na pamoja na vijana, kwa nini wasiwe kinababa? Ni kwa sababu vijana mnaweza kukimbizana na wakati na kinamama mnajukumu la kulea familia wakiwemo kinababa,” alisema Anna na kushangiliwa na kinamama kwa makofi na vigelegele.
Aidha,Mkurugenzi wa Taasisi ya “Creative Plan” yenye kali mbiu ya SEMA USIKIKE, ndugu Juma Mtetwa akasema, “…tumekubali kuairisha safari na kujumuika nanyi hapa kwa jinsi juhudi za Mkurugenzi Ngatunga zinavyoonekana na mimi huwa napenda kumuita Digital, najua anavyosikiliza na anavyotenda, mpigieni makofi makubwa sana.” Baada ya kusema hayo aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi hasa katika tukio la jana la Uzinduzi wa Sema Usikike.
Nae mwanakikundi Dada Asha Mgaywa ambae kikundi chao cha Tumaini kilichopo Kata ya Mole Wilayani Sikonge kimesifiwa kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kurejesha fedha hizo za Mikopo, alisema haya, “ Sisi kama wanakikundi tumejiwekea utaratibu wa kukutana na kujadili namna ya kufanya biashara ili tuweze kufanikiwa kutokana na fedha tunazokopa lakini pia tunapeana mawazo na kutiana moyo na hii ndio siri kubwa ya mafanikio yetu.”
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa