SHULE BINAFSI KILIO CHA WENGI-SIKONGE.
Wawezeshaji kutoka ESRF waliokaa kulia wakijadiliana na wajumbe kwenye semina ya fursa za uwekezaji iliyofanyika Ofisi ya Mkurugenzi - Sikonge.
Timu ya wawezeshaji kutoka Shirika la Economic and Social Research (ESRF) yatua Sikonge kujadili fursa za uwekezaji.
Timu hiyo iliyoundwaa na wajumbe watatu akiwemo Dr. Bohela Lunogelo, Ben Mtalemwa na Prof. godwin Mjema, ilifanikiwa kukutana na wawakilishi wa wafanyabiashara, wakuu wa Idara pamoja na vitengo vilivyopo Wilayani hapa na kufanya semina iliyolenga kubainisha fursa zinazoweza kutumiwa na wadau wanaohitaji kuwekeza Wilayani Sikonge.
Miongoni mwa fursa iliyopewa kipaumbele na wajumbe waliohuzulia semina hiyo ilikuwa ni uanzishwaji wa shule binafsi za msingi zinazotumia mtaala uliokwenye lugha ya kiingereza ambapo wajumbe 10 walichangia kuwa ni miongoni mwa jambo linalopewa kipaumbele kikubwa. Wilaya ya Sikonge haina shule ya namna hiyo hata moja jambo linalowalazimu wazazi kuwapeleka watoto wao nje ya Wilaya hii na hata mikoa mingine ikiwemo Shinyanga- Kahama.
Hali hii imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa Sikonge ambao wamekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo, hivyo kuwakaribisha wadau wote wenye uwezo wa kuwekeza katika shule binafsi kuchangamkia fursa hiyo.
Akielezea kivutio kinachopatikana katika uwekezaji huo Martin Ukongo ambaye ni Afisa Ardhi alisema kuwa gharama za upatikanaji wa eneo zipo chini kulinganisha na sehemu zingine na tayari Halmashauri imetenga eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji huo ambapo ili kuwavutia wawekezaji mita moja za mraba huuzwa kwa thamani ya shilingi elfu moja tu.
Mbali na fursa hiyo pia kulijadiliwa fursa mbalimbali zinazopatikana Wilayani hapa ambazo miongoni mwao zilikuwa ni kujenga kiwanda kwa ajili ya mazao ya Nyuki, kilimo cha Umwagiliaji, kiwanda cha Mafuta, Hoteli na huduma za kitalii na uanzishaji wa Mashamba makubwa ya Tumbaku, Alizeti na Karanga, ambapo zinaweza kutumiwa na wawekezaji kwani maeneo yapo ya kutosha.
Majadiliano yakiendelea- Semina ya Fursa za Uwekezaji Sikonge.
Akitoa maelezo namna Sikonge inavyoweza kuzitangaza Fursa zilizopo, muwezeshaji Dr. Bohela Lunogelo alisema kuwa mawazo yote yaliyotolewa na wadaau yatawekwa kwa pamoja na machapisho mbalimbali yatatolewa ili yaweze kuwafikia wadau wa uwekezaji, pia alishauri kutumia machapisho na makala ambazo zitarushwa kwenye mtandao wa kijamii lengo likiwa ni kufikisha ujumbe sehemu mbalimbali kama njia ya kuwakaribisha wawekezaji.
Naye injinia Paschal Ngunda aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi alitoa shukurani kwa wawezeshaji kutoka ESRF kwa kusema, “mambo mengi hayafanikiwi kwa kuwa hayana miongozo sahihi” hivyo alishukuru timu hiyo kwa kuwapa miongozo sahihi itakayofungua fursa za uwekezaji Wilayani Sikonge.
IMEANDALIWA NA
KITENGO CHA TEKNOLOJIA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
SIKONGE.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa