Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na uboreshaji wa huduma ya afya kwa umma(MDH) limeendesha mafunzo kwa waheshimiwa madiwani,watendaji wa kata pamoja na watendaji wa vijiji juu ya elimu ya afya katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Bw.Simon Malley,Afisa takwimu toka MDH amesema upo umuhimu kwa viongozi katika kata na vijiji kutilia mkazo suala zima la afya ya akinamama wajawazito kutokana na changamoto za kuanza kliniki ya ujauzito kwa wakati pamoja na kufanya kipimo cha marudio .Amesisitiza ni muhimu kuhamasisha na kuelimisha kuhusu jambo hilo ili kuwalinda wanawake na changamoto za uzazi.
Kwa upande wake Bi. Veronica Ferdinand,Afisa lishe wilaya ya Sikonge amesisitiza umuhimu wa lishe bora kwa mtoto ili kuepukana na athari za udumavu ambazo huathiri sana watoto katika makuzi na utendaji wao darasani,hivyo amesisitiza umuhimu wa wazazi kuzingatia mlo wa mtoto. “Mtoto anayekua anahitaji kula si chini ya mara tano kwa siku na sio kula tu bali kula chakula chenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji wake.” Amesema Bi. Veronica.
Akiwasilisha mpango mkakati kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto,Mratibu wa Afya ya uzazi na mtoto Bi. Lenatha Mondo amesema moja ya njia ya kuimarisha afya ya mama na mtoto ni pamoja na kuboresha elimu ya afya ya uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya,huduma za mkoba zifanyike katika maeneo yasiyoweza kufikika kirahisi pamoja na maeneo ambayo hayana vituo vya kutolea huduma za afya na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa na kukomesha huduma za upimaji na kuzalisha zinazofanywa kinyume na utaratibu katika maduka haya.
Aidha mada zingine zilizowasilishwa ni pamoja na elimu juu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.Bado ipo haja ya kuiunga mkono Serikali katika mapambano inayoyaongoza dhidi ya ugonjwa huu wa hatari hasa kwa kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na kuzuia maambukizi mapya katika jamii kwa ujumla.
Akifunga mafunzo hayo Mhe. Rashid Magope,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ametoa wito kwa shirika la MDH kupanua wigo ili kuwafikia viongozi wengi zaidi hasa waheshimiwa madiwani kwani uwakilishi wao na ushawishi wao katika maeneo yao utasaidia sana katika kuleta mwamko juu ya afya ya mama na mtoto kwa haraka.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa