SERIKALI YAWAJALI WALIMU
Kata ya Usunga iliyopo Wilayani Sikonge ni miongoni mwa kata zilizofaidika na miradi ya TEA ambapo katika shule ya Sekondari Usunga wamejengewa nyumba bora ya waalimu ijulikanayo kama six in one.
Hivi karibuni kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ikiongozwa na Mhe. Peter Nzalalila ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri walitembelea shuleni hapo na kukagua ujenzi huo ambao tayari umekamilika na hatua za kwanza za kukabidhi kwa Muhandisi wa Wilaya zilikuwa zimekamilika.
Wakiwa katika ukaguzi wa Nyumba hiyo wajumbe wa kamati ya fedha walitoa pongezi mbalimbali kwa serikali ya awamu ya tano ilivyojitolea kuwajali watumishi wake kwani kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa watumishi.
Mhe. Nzalalila alitoa maagizo kwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari usunga kuhakikisha inafanya utaratibu wa kuwapata walimu sahihi ambao watapewa nyumba hizo ili waanze kuzitumia. Akiongeza “kusiwe na upendeleo kwenye ugawaji wa nyumba hizo wapewe wanaostahili”.
Akichangia swala hilo Mhe. Zena Aruna ambaye ni diwani viti maalumu CCM alisema kuwa serikali imetoa pesa nyingi katika mradi huo hivyo mtumishi yeyote atakayekabidhiwa nyumba hiyo ni jukumu lake kuhakikisha anaitunza vizuri na kwa kuzingatia usafi, “hatutavumilia kuona mazingira ya nyumba hii yanaharibiwa, mtumishi yeyote atayepewa nyumba hii ahakikishe anaitunza kama anavyotunza nyumba yake”.
Akitoa pongezi zake kwa serikali Mwenyekiti wa ujenzi wa nyumba hiyo alisema kuwa mradi huo umenufaisha wazawa kwani ulikuwa ni chanzo kizuri cha ajira kwa wakazi wa eneo hilo.
Sanjari na hayo mradi huu pia utasaidia katika kuinua kiwango cha ufauru shuleni hapo kwani utawaweka walimu karibu na mazingira yao ya kazi jambo litakalosaidia kuwa karibu na wanafunzi na kugundua kwa haraka mabadiliko yeyote yatakayojitokeza.
baadhi ya wajumbe wa kamati ya Fedha wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kamati ya ujenzi nyumba ya walimu kata ya Usunga.
“Hatutakubali mwalimu amepewa nnyumba nzuri namna hii alafu atoe wanafunzi wenye ziro” alisema Mhe. Juma Mdulla akitoa onyo kwa walimu wa shule ya sekondari Usunga.
Kamati hiyo ilitoa pongezi nyingi kwa raisi wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwa karibu na wananchi wake na kuwajali watumishi, pia kwa mbunge wa jimbo la Sikonge Mhe. Joseph Kakunda kwa kutimiza ahadi zake na pia waliwaasa wananchi kuwa wanajitolea katika miradi inayokuja kwasababu inawagusa wao moja kwa moja.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa