SEKTA BINAFSI ZINAZOSAMBAZA NISHATI YA UMEME VIJIJINI ZAAGIZWA KUZINGATIA BEI ELEKEZI.
Sekta binafsi zilizopewa kibali cha kuzalisha nishati ya umeme zaagizwa kufuata bei elekezi iliyotolewa na Serikali wakati wa kuuza vifaa vya umeme pamoja na usambazaji wa Umeme kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu alipofanya ziara Wilayani Sikonge ili kukagua namna ambavyo mradi wa Umeme Vijijini (REA) unavyowasaidia wakazi wa vijijini, na kufanikiwa kutembelea vijiji vya Kikungu kata Chabutwa, Kata ya Ipole na Kijiji cha Lukula kilichopo kata ya kitunda ambacho kinapata umeme wa Jua.
Akitoa bei elekezi Mhe. Mgalu Alisema kuwa mwananchi atachangia shilingi elfu ishirini na saba (27,000/=) tu ili kupata nishati ya umeme lakini gharama za kusambaza nyaya katika nyumba (wirering) zitakuwa juu ya mteja mwenyewe na baada ya hapo atavutiwa umeme na sio vinginevyo.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu (Mwenye Mtandio Mwekundu) alikata utepe kuashiria uzinduzi wa nishati ya umeme kuanza kutumika katika msikiti uliopo kijiji cha Kikungu Kata ya Chabutwa Wilayani Sikonge.
Akiwa kata ya Kitunda pia alifanikiwa kukagua mradi wa PowerCorner ulio chini ya sekta binafsi ambao unazalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua, na kumtaka muwekezaji huyo kutoa huduma kwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na serikali kwasababu serikali iliingia ubia na kampuni hiyo kwa kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 3 ili kufaniisha mradi huu. Vilevile alipita kukagua namna ambavyo mradi huo umekuwa fursa kwa wananchi kujikwamua kiuchumi ambapo alizungumza na mafundi wa kuchomelea chuma wanaotumia nishati hiyo.
Sanjari na hayo pia Mhe. Mgalu aligawa Swichi ya Umeme aina ya uwamita kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni mpango wa serikali kuwasaidia wenye ulemavu, wajane na wazee wenye umri mkubwa ili nao waweze kupata nishati ya umeme. Huku akiitaka EWURA kujenga utaratibu wa kuwatembelea wananchi wa vijijini mara kwa mara ili kubaini changamoto na kuzitatua mapema.
Katika ziara hiyo pia aliambatatana na wenyeji wake akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Peter Nzalalila, Mkurugenzi Bi. Martha Luleka, Katibu Tawala Wilaya Renatus Mahimbali pamoja na mbunge wa jimbo la SIKONGE Mhe. Joseph Kakunda ambaye alitoa shukrani zake kwa serikali kwa kuwatoa wananchi gizani kwani wamekuwa wakisubiri kupatiwa nishati ya umeme kwa muda mrefu na sasa umeme unawaka hadi majumbani.
Vilevile aliongeza kuwa wananchi waitumie fursa hiyo vizuri ili kujiendeleza na shughuli za kiuchumi, kwani utawasaidia kurahisisha kazi zao sambamba na kuongeza muda wa kufanya kazi.
Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ilikuwa ni kijiji cha kikungu ambapo alizindua umeme katika ofisi ya Mtendaji wa Kata, Nyumba ya Mzee Issa pamoja na Nyumba ya Ibada (Msikiti) pamoja na kukabidhi Swichi kwa Mtu mwenye ulemavu.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa