RC MWANRI ATAKA USIMAMIZI MAKINI MIRADI YA MAENDELEO SIKONGE
Na Eveline Odemba, Sikonge
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameagiza Wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge kufuatilia utekelezakaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo kwa umakini mkubwa ili kuepusha udanganyifu.
Alitoa agizo hilo juzi alipofanya ziara maalumu ya ukaguzi wa miradi ya shule inayotekelezwa katika na serikali katika halmashauri hiyo.
Akiwa katika shule ya Msingi Ulilwansimba alikagua ramani za majengo na kugundua kuwa ramani haikufuatwa hasa katika jengo la vyumba viwili vya madarasa ambapo ramani yake ilionesha kuna chumba cha ofisi ya walimu lakini kwa namna lilivyojengwa hakuna ofisi hiyo.
Alibainisha kuwa kukosekana kwa ufuatiliaji makini wa miradi inayotekelezwa na Serikali katika halmashauri ndiyo chanzo cha uharibifu wa miradi, hivyo akaagiza Ofisa Elimu wa shule za msingi na Kaimu Mhandisi wa wilaya hiyo kufuatilia kila hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Aliagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Martha Luleka kuwasiliana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuomba kupatiwa Mhandisi mwingine wa ujenzi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi hiyo baada ya aliyekuwepo kuhamishiwa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijiji (TARURA).
Mhe. Agrey Mwanri Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliyevaa shati rangi ya Bahari akitoa maelekezo alipotembelea miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Wilayani Sikonge.
‘Sikonge mnafanya vizuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo tatizo lililopo ni kukosekana kwa umakini katika ufuatiliaji, ndiyo maana wakandarasi wanafanya wanavyotaka, wataalamu kuweni makini sana’, alisema.
Aidha Mkuu wa Mkoa alitembelea shule ya Sekondari ya Kamagi ambapo alisisitiza suala la kubana matumizi katika utekelezaji miradi hiyo sambamba na kuangalia ubora wa vifaa vinavyotumika.
Ili kufanikisha miradi hiyo alipendekeza kufuatwa kwa ramani iliyopo ikiwemo kuhakikisha matofali yanamwagiliwa asubuhi na jioni ili kupata ubora unaohitajika huku akiwataka kutokata miti ovyo kuhakikisha mfumo wa maji na umeme unawekwa kabla ya jengo kupigwa plasta.
Aidha alimwagiza Ofisa Elimu Sekondari Yusuph Hamza kuhakikisha mbao zisizo na ubora zinarudishwa kwa muuzaji kwani hazifai kutumika.
Akijibu hoja hiyo Kaimu Mhandisi wa Wilaya Bi. Joyce Faustine alisema kuwa walichukua maamuzi ya kuamishia ofisi kwenye jengo la pili kutokana na kuwa jengo la kwanza kupakana na jengo la zamani ambalo ofisi tayari ilikuwepo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri alishukuru kwa niaba ya Wilaya na kuahidi kutekeleza yale yote yaliyoagizwa na Mkuu wa mkoa huku akibainisha kuwa ataweka kambi katika Shule ya Kamagi ili kuhakikisha fedha zilizotolewa na serikali zinatumika vizuri na mradi unakamilika kwa wakati.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa