Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amezuru Wilayani Sikonge akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kusikiliza na kutatua kero za Wakulima wa Tumbaku hususani katika Kata ya Kisanga.
Akifungua kikao hicho Mhe. Balozi Burian amesema kilichosababisha kuja Sikonge ni baada ya kujitokeza kwa sintofahamu katika Chama cha Amcos Kisanga hasa baada ya kuuza tumbaku yao na wakulima kushindwa kupokea malipo ya jasho lao kwa sababu ya deni linalowakabili katika benki ya NMB Sikonge.
Mhe.Burian amesikitishwa sana na mwenendo wa kilimo cha tumbaku Sikonge hasa baada ya kuona jinsi wakulima walivyojituma kwa juhudi na kuishia kulipa madeni tu.
Akiongoza kikao hicho kilichohudhuriwa na wakulima pamoja na viongozi wao amesema haki ya wale waliolima lazima ipatikane “Hatuwezi kuwavumilia watu wanao wadhulumu wakulima” amesema Balozi Batilda.
Kwa upande wao wakulima wakiwasilisha malalamiko yao mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora wamesema Chama cha Msingi Amcos Kisanga hakijawalipa wakulima haki yao na hii inasababishwa na kuwa na deni kubwa benki wanakochukua ruzuku,lakini pia kuna wakulima wasio waaminifu wanaochukua ruzuku lakini baada ya kuvuna tumbaku hukimbilia kuuza tumbaku soko huria hivyo kusabisha deni kubwa la fidia ya ruzuku kwa wakulima waaminifu.
Aidha imebainika kuwa viongozi wa chama cha msingi Amcos Kisanga kutumia madaraka yao vibaya kwa kushiriki kuuza tumbaku nje ya chama cha msingi lakini pia kushidwa kuwasomea deni wanalodaiwa wakulima katika chama cha Amcos Kisanga.
Baada ya kuwasikiliza wakulima na changamoto zao Mhe. Mkuu wa Mkoa aliahirisha kikao na kuamuru mara moja kuketi kama kamati ya uchunguzi ya mkoa ili kuleta suluhu ya kero zinazowakabili wakulima hao.
Baada ya kamati ya uchunguzi kuketi Zaidi ya masaa Matano ikiongozwa na Mhe. Dkt. Burian imebaini mambo Matano,Utoroshaji mkubwa wa tumbaku ili kukwepa kulipa deni la chama cha msingi,Changamoto katika chama cha Kisanga Amcos,imebaninika kumekuwa na utakatishaji mkubwa wa fedha,Ukopeshaji wa pembejeo wenye upendeleo,Utoaji mikopo wenye upendeleo,utoaji wa pembejeo usiozingatia uwezo wa mkulima,Udhaifu katika usimamizi wa tumbaku toka kwa Afisa ushirika na matumizi mabaya ya madaraka hasa katika kufanya maamuzi mbalimbali.
Akifunga kikao hicho Dkt. Burian ameamuru watumishi watano wanaohusika na masuala ya chama cha msingi Amcos na ushirika kuwekwa chini ya ulinzi ili kusaidia uchunguzi wa kero zilizobainika.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa