Na Edigar Nkilabo – SikongeDC
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imewapatia Watendaji 10 wa Vijiji pikipiki za mkopo usiokuwa na riba kwa lengo la kuwawezesha kufika kwa wakati katika Vitongoji vyao na kutoa huduma bora kwa wanachi wa maeneo yao.
Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi pikipiki hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndugu Selemani Pandawe amesema programu hii inalenga kutatua changamoto ya usafiri kwa Watendaji wa Vijiji.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tumeanza na hizi pikipiki 10 kwa kuwapatia Watendaji wa Vijiji wenye maeneo makubwa na yambali lengo ni kuwawezesha kufanya kazi ya serikali kwa wepesi na baadae watakapomaliza mkopo na kutunza chombo hiki vizuri tutahamisha umiliki kutoka Halmashauri na kuwa pikipiki zao”amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali Watu Ndugu Nico Kayange amesema Mpango huu wa ununuzi wa Pikipiki za mkopo usiokuwa na riba ulianza na Watendaji wa Kata na baada ya kukamilisha marejesho , Halmashauri imeagiza pikipiki zingine 10 kwaajili ya Watendaji wa Vijiji.
“Tulianza kutatua changamoto ya usafiri kwa Watendaji wetu wa Kata na sasa tumeanza kuwakopesha Watendaji wa Vijiji ili na wao waweze kuyafikia maeneo yao ya kiutendaji kwa wakati na kutoa huduma”
“Pikipiki zote 10 tulizonunua zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 35 na chimbuko la fedha hii ni fedha iliyobaki baada ya kununua gari ya Mkurugenzi Mtendaji ndipo menejimenti ilipoamua kununua pikipiki na kuwakopesha Watendaji wetu , tukianza na wale wa Kata na sasa tunawapatia hawa wa Vijiji ambao wataulipa mkopo huu kwa kipindi cha miaka 2 kisha kukabidhiwa moja kwa moja pikipiki hizo”amesema.
Kwa uapnde wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga ameipongeza Halmashauri kwa ubunifu huo wa kutatua changamoto za usafiri kwa Watendaji wake wa Kata na Vijiji kwani fedha hiyo ingeweza kupangiwa matumizi mengine.
“Binafsi niwapongeze kwa kuamua kuwasaidia usafiri Watendaji wetu maana Jiografia ya Wilaya yetu ni kubwa utendaji wake bila usafiri ni mgumu, fedha hizo baada ya kubaki kwenye ununuzi wa gari ya Mkurugenzi Mtendaji mngeweza kufanyia shughuli nyingine lakini kwakuwajali Watendaji wetu mkaona mtatue changamoto ya usafiri ili wakatoe huduma bora kwa wananchi wetu”amesema Mhe.Myinga.
Aidha Mhe.Myinga amewataka Watendaji wa Vijiji kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa manufaa ya umma na binafsi kwakuwa mkataba uko wazi baada ya marejesho watapewa umiliki wa pikipiki hizo.\
“Mtunze hivyo vyombo vya moto kama mali yenu ili baada ya kukamilisha malipo muwe na kumbukumbu lakini pia muendeshe kistaarabu haina haja ya kukimbia sana , ukikimbia sana ukianguka na pikipiki utapoteza maisha au kuwa mlemavu”amesisitiza.
Akishukuru kwa niaba ya Watendaji wa Vijiji waliopata pikpiki hizo Ndugu Enock Mangu Mtendaji wa Kijiji cha Idekamiso amesema wanaishukuru sana Halmashauri kwa kuwapatia pikipiki hizo kwani zitawarahisishia kazi kwa kufika katika Vitongoji vyao na kutoa huduma kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa