Robert Magaka – Sikonge.
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali imeendesha mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi kwa viongozi na makundi mbali mbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwanambuya Sikonge.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Salha Burian amesema mafunzo hayo yanalenga kutoa mrejesho wa kazi iliyofanyika nchi nzima iliyoanza kwa zoezi la anuani za makazi na baadaye sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Matokeo ya Sensa ya watu na makazi yameonesha kuwa Mkoa wa Tabora unashika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuwa na idadi kubwa ya watu 3,391,679 wanaume wakiwa 1,661,171 na wanawake 1,730.508.
Na kwa upande wa matokeo ya idadi ya watu Kiwilaya, Sikonge ina jumla ya watu 335,686 ikiwa wanaume ni 165,309 na wanawake 170,377.
Aidha Mhe. Burian ametoa wito kuwa Taarifa za sensa ya watu na makazi zitumike kwa ajili ya kuleta maendeleo ya watu katika maeneo yao. “Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea watu uwezo wa kutafsiri na kuchambua na kuyatumia matokeo ya sensa katika kupanga,kutekeleza na kufuatilia tathmini ya utekelezaji wa sera na mipango yetu kwa muda mfupi,muda wa kati na muda mrefu” amesema Dkt. Burian.
Akimwakilisha Mtakwimu Mkuu wa Serikali Meneja Idara ya Mifumo ya Kijiografia Ofisi ya Takwimu Taifa Bw. Benedict Mugambi amesema Serikali imekamilisha kuandaa na kuzindua ripoti 11 za sensa ikiwa ni pamoja na matokeo ya mwanzo,ripoti hizi zimejikita katika mgawanyo wa idadi ya watu kwa maeneo ya kiutawala hadi ngazi ya kata au shehia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ripoti ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa majimbo ya uchaguzi Tanzania bara na Visiwani.
Akifunga mafunzo hayo Mhe. Dkt. Burian amepokea na kujibu baadhi ya hoja na Changamoto zilizowasilishwa na wanachi waliohudhuria mafunzo hayo na hoja zingine ameahidi Kwenda kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na ombi la wanasikonge kuongezewa jimbo lingine la uchaguzi,uharibifu wa miundo mbinu ya Barabara na ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo mengi ya Wilaya ya Sikonge.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa