Akiongoza kikao cha Usafi wa Mazingira kwa Kata ya Sikonge na Misheni kilichowahusisha Watendaji wa Kata husika ,Afisa Tarafa,Maafisa Mazingira pamoja na Afisa Afya wa Wilaya,Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Simon Chacha amesema ni muhimu kila mtu akasimamie usafi wa mazingira kwa mamlaka aliyopewa katika eneo lake na kwamba amedhamiria sikonge kuwa mji safi.
DC Chacha amesisitiza sana kuelimisha wananchi juu ya suala la usafi wa mazingira kwani usafi ni jambo la msingi ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kuhara.
Vilevile amewasisitiza watendaji wa kata za Sikonge na Misheni Kwenda kufanya kazi kwa bidii na kwa kujiamini na kutumia mamlaka yao ipasavyo ilimradi hawamuonei mtu.
Kwa upande wake Afisa Afya Wilaya Bw. Laurent Lushekya akichangia hoja katika kikao hicho ameeleza kuwa wanakwenda kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayebainika kutotekeleza agizo la serikali kuhusu agenda ya usafi wa mazingira hususani ujenzi wa vyoo bora katika makazi yao.
Naye Mhe. Diwani wa Kata ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila amemuahidi Mhe. Chacha kuwa watamuunga mkono katika juhudi zake za kuhakikisha mji wa Sikonge unakuwa safi. “Sisi tuko pamoja na wewe katika suala hili hatutakuangusha” amesema Mhe. Nzalalila.
Akifunga kikao hicho Mhe. Chacha ameagiza viongozi wote wakatekeleze agenda ya usafi kwa kushirikiana na atapita na timu yake katika maeneo ya mji wa Sikonge ili kuona utekelezaji wa zoezi la usafi wa mazingira linavyofanyika.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa