MWENGE WA UHURU WAZINDUA ZAHANATI YA KISASA SIKONGE
Na Evelina Odemba, Sikonge
MBIO za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2019 zimezindua mradi wa Zahanati ya kisasa uliotekelezwa na Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora kwa gharama ya zaidi ya Shilingi mil. 261.6 katika kijiji cha Kikungu kata ya Chabutwa.Zahanati hiyo inayotarajia kunufaisha wakazi zaidi ya 7,000 wa kata ya Chabutwa na kata jirani za Ipole na Kipanga ni ya kipekee katika wilaya hiyo kutokana na kutekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Mtendaji wa Kijiji Salome ........ akisoma taarifa ya Mradi wa Zahanati hiyo wakati wa Uzinduzi, pembeni ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sikonge Martha Luleka.
Akizindua Zahanati hiyo jana, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mzee Mkongea Ally alisema kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mizuri yenye manufaa makubwa kwa wananchi. Aliwataka akinamama wajawazito na wenye watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka 5 na jamii kwa ujumla kutumia Zahanati hiyo ipasavyo kwa kuleta watoto wao kliniki na kwenye chanjo ili wapate huduma za afya.
Mkongea alisema kuwa utekelezwaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa katika halmashauri zote hapa nchini ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya. ‘Mama zetu msiende kwa waganga wa kienyeji, mtapoteza maisha yenu na watoto, tumieni ipasavyo zahanati na vituo vya afya vilivyojengwa na Serikali katika maeneo yenu’, alisema. Aliitaka jamii kuendelea kumuunga mkono Rais Dakt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya katika awamu hii ya utawala wake ili aendelee kufanya zaidi kwa manufaa ya wananchi wote wa taifa la Tanzania.
Naye Mkuu wa wilaya ya Sikonge Peres Magiri alibainisha kuwa kufunguliwa kwa zahanati hiyo kutasaidia sana kupunguza vifo vya mama na mtoto na kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 7,000 wa vijiji 5 vya kata hiyo na kata jirani. Katika taarifa yake Mtendaji wa Kijiji hicho Salome............ alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo umegharimu kiasi cha shilingi mil. 261.6 ambapo Serikali kuu imechangia shilingi mil. 138.6, Halmashauri shilingi mil. 116.9 na wananchi shilingi mil. 6.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Nzalalila alisema zahanati hiyo imejengwa kwa ajili ya wananchi, hivyo akawataka wakazi wa vijiji vyote vya kata hiyo na kata jirani kwenda kupata matibabu wakati wowote wanapohitaji huduma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa