Na Edigar Nkilabo
Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe.Paul Chacha amewataka Wakuu wa Wilaya za Sikonge na Tabora Mjini walioteuliwa na kuapishwa kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi watakaowakuta ili kuleta matokeo chanya katika maeneo yao pamoja na kuendeleza mazuri ya watangulizi wao.
Mhe.Paul Chacha ametoa kauli hiyo katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwana Kiyungi wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Wilaya za Sikonge na TaboraMjini ambapo amewataka kuwatumikia wananchi wa maeneo yao kama watangulizi wao walivyofanya.
“Nikiwatazama hapa naona nyote ni wachapa kazi hakuna legelege hata watangulizi wenu walikuwa wanafanyakazi vizuri ya kuwahudumia wananchi hakuna ambaye ameondoka kwa kufukuzwa bali ni uchapa kazi wao ambao umewafanya wakapambane katika nafasi zingine nanyi bebeni mema myaendeleze”alisema.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt.John Mboya amewasisitiza viongozi hao wapya kusimamia maadili ya utumishi wa umma na kuzingatia viapo vyao ili kufanya kazi kwa weledi na ufanisi pindi wanapowahudumia wananchi.
“Hkikisheni mnapotekeleza majukumu yenu mnazingatia sheria,kanuni na taratibu za kazi kuepuka mtafaruku katika utendaji, pia tangulizeni uzalendo mkawasikilize wananchi na kutatua changamoto zao kwa wakati”alisema Dkt.Mboya.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Tabora Ndugu Said Nkumba amesema Chama kimewapokea kwa mikono miwili na watatoa ushirikiano kwa viongozi wote kuhakikisha wanawaletea maendeleo wananchi.
“Sisi tutatoa ushirikiano kwa viongozi wapya kuhakikisha mambo yanaenda, Chama hiki kinachotawala adhima yake ni kutoa huduma kwa Watanzania na hayo ndiyo matarajio ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan”alisema.
Kwa upande wao Wakuu wa Wilaya wapya wamesema wako tayari kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanachi wanapata huduma bora.
“Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii, mimi ni msaidizi wako niko tayari kufuata maelekezo yako na kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Sikonge”alisema Mhe.Thomas Myinga Mkuu wa Wilaya ya Sikonge.
Hafla hiyo ya uapisho imeambatana na zoezi la kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wote wapya walioteuliwa na Mhe.Rais katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya, Wakuu wa Wilaya na Katibu Tawala.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa