Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe.Paulo Chacha amefanya ziara ya kutembelea mgodi wa kitunda uliopo kata ya Kitunda wilayani Sikonge pamoja na kusikiliza kero za wananchi wa eneo hilo.
Akiwasilisha changamoto zinazowakabili wachimbaji wa mgodi huo, Katibu wa Chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Tabora (TABOREMA) Godfrey Mwaniwiti amesema wachimbaji wa mgodi huo wanachangamoto ya ukosefu wa mashine ya kisasa ya kuchoronga miamba ya madini hali inayoathiri uzalishaji wa madini kwakuwa wachimbaji wengi hufanyakazi kwa kubahatisha.
“Wachimbaji wengi tunafanyakazi kwa hisia kwakuwa hatuna mitambo ya kisasa ambayo ingetuwezesha kuongeza uzalishaji wa madini kama baadhi ya wachimbaji wa mikoa mingine hivyo serikali itusaidie hiyo mitambo na sisi tuchimbe kwa tija”alisema.
Akitoa jawabu la changamoto hiyo Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Bi.Fatuma Kyando amesema Wizara ya Madini chini ya Kampuni ya STAMICO tayari imenunua mashine za kisasa za kuchoronga.
“Katika awamu ya kwanza mashine hizo zilisambazwa katika mikoa michache kwa mkoa wa Tabora tutapata mashine hizo awamu ya pili ambacho wachimbaji mtatakiwa kufanya ni kuchangia gharama kidogo ili kuzitumia mashine pindi zitakapofika’’alisema.
Akijibu baadhi ya kero za wananchi, Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe.Paulo Chacha amewataka wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la hifadhi la Kalulu Inyonga East na badala yake waenedelee kuchimba katika maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Ni marufuku kuanzia leo kwa mchimbaji yeyote kwenda kuchimba madini katika eneo la hifadhi na wale wote waliokata leseni katika maeneo ya hifadhi leseni hizo zimefutwa atakayeingia humo akikamatwa sheria itafuata mkondo wake”alisema.
Aidha Mhe.Chacha amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi katika eneo la mgodi wa Kitunda,pamoja na mifuko mingine 50 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo cha polisi.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Cornel Magembe ameunga mkono juhudi za wananchi hao kwa kuchangia mifuko mingine 50 ya saruji ili kukamilisha kituo hicho cha polisi kwa lengo la kuimarisha usalama kwa wakazi wa eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa