MKUU WA MKOA WA TABORA AKAGUA MRADI WA UJENZI WA WODI TATU KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA SIKONGE
Na Anna Kapama
21 Aprili, 2021
Mkuu wa MKOA wa Tabora Dkt.Philemon Sengati amefanya ziara Wilayani Sikonge leo na kukagua mradi wa ujenzi wa majengo matatu ya Hospitali ya Wilaya ya Sikonge ikiwemo Wodi ya kina mama, wanaume na wodi ya wazee na kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo ambao umeanza mwezi wa nne mwaka 2021.
Aidha, Dkt.Sengati amewapongeza viongozi na wasimamizi kwa kusimamia vizuri mradi huo.
Pia, Mkuu wa mkoa amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sikonge, Tito Luchagula kwa kuwasimamia vyema viongozi na idara zinazohusika katika ujenzi huo akiwapa viapaumbele mafundi ujenzi wanaopatikana Wilaya ya Sikonge na kuongeza kuwa ni jambo jema kuwapa fursa hizo kwa kuwa itakuza ujuzi na maendeleo binafsi kwa wakazi hao.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewataka watoa huduma za afya Wilayani hapo kuzingatia na kufuata taratibu sheria na kanuni za utoaji wa huduma za afya,huku akisisitiza matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa.
Aidha,katika utoaji wa huduma za afya bure kwa watu wenye makundi mbalimbali wakiwemo wajawazito,wazee na watoto chini ya umri wa miaka mitano, Dkt.Sengati amesema wapatiwe huduma hizo kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na kuongeza kuwa wasitozwe gharama yoyote.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Sikonge, Renatus Mahimbali akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ameishukuru Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya,huku akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya Ziara katika Wilaya hiyo na kuongeza kwamba uongozi utasimamia vyema miradi yote ya maendeleo.
Mradi huu wa ujenzi wa majengo matatu katika Hospitali ya Wilaya ya Sikonge utagharimu Shilingi Milioni 500 mpaka kukamilika kwake,na baada ya kukamilika utaongeza ufanisi katika kutoa huduma za Afya na kupunguza vifo visivyo vya lazima Wilayani hapa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameambatana na Katibu Tawala Mkoa, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Mhandisi wa Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi Mipango, Mhasibu Mkoa na Waandishi wa Habari.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa