Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 zikiongozwa na kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava,zimewasili wilayani Sikonge zikiangazia miradi nane ya maendeleo yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni moja.
Mradi wa kwanza uliomulikwa na Mwenge wa uhuru ni ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mkolye, ambayo inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 175.4, itachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo. Ujenzi wa zahanati utapunguza usumbufu wa safari ndefu za kutafuta huduma za afya na kuimarisha hali ya afya ya jamii.
Katika mbio hizo, Mwenge ulifungua ukurasa mpya katika sekta ya utalii kwa kuwekwa jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba ya kulala wageni ya Madiba Lodge. Ujenzi huu utahakikisha kwamba eneo hilo linakuwa na miundombinu bora ya kulaza wageni, jambo ambalo litachochea maendeleo ya utalii na kutoa ajira kwa wakazi wa Sikonge.
Shughuli nyingine muhimu zilizofanywa na Mwenge wa uhuru ni uwekaji wa jiwe la msingi katika matengenezo maalum ya barabara ya kiwango cha lami kutoka Misheni hadi Hospitali ya Moravian, kwa umbali wa kilometa 0.55. Barabara hii itarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, na kuimarisha uunganishaji wa maeneo muhimu ya kijamii.
Mbali na hayo, Mwenge wa Uhuru umeleta matumaini kwa vijana kwa kuweka jiwe la ufunguzi katika ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika shule ya sekondari ya Kiwere. Hii itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kutoa fursa bora za elimu kwa wanafunzi wa eneo hilo.
Mbio za Mwenge wa uhuru zinafikia tamati leo kwa mkoa wa Tabora,zikiwa zimeweza kuchochea maendeleo katika sekta za afya,elimu,miundombinu na ustawi wa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa