Na Edigar Nkilabo
Kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa shule ya awali na msingi Mpandepande iliyopo katika kijiji cha Kiyombo kata ya Kipili wilayani Sikonge watoto zaidi ya 700 kutoka kijijini hapo wamefutwa machozi ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu hali inayotajwa kupunguza msongamano darasani pamoja na kuwanusuru wanafunzi na tabia ya utoro.
Mbunge wa Jimbo la Sikonge Mhe.Joseph Kakunda akizindua shule hiyo, amesema serikali ya awamu ya sita ni sikivu kwani alipoomba fedha za ujenzi wa shule hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 300 kwa haraka zilitolewa na ujenzi kuanza jambo ambalo limeongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
Mhe.Kakunda amewasisitiza wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kupeleka watoto shule ya awali na msingi ili wapate haki yao ya kikatiba.
“Tayari serikali imetusogezea shule karibu kazi yetu ni moja tu, kupeleka watoto shule wakasome uzuri mazingra ni mazuri shule imejengwa kisasa hatuna kisingizio kingine zaidi ya kutimiza wajibu wetu” amesema.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe.Rashid Magope amewataka Walimu na Wanafunzi wa shule ya Msingi Mapandepande iliyopo Kata ya Kipili kuitunza miundombinu ya shule hiyo ili idumu na kutoa huduma kwa wanafunzi wa Kata hiyo ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kuyatafuta maarifa.
Naye Afisa Elimu Taaluma elimu ya Awali na Msingi Ndg. James Mayala amesema ni wajibu wa wazazi na walezi kupeleka watoto shule ili wapate elimu bora kwakuwa serikali inawekeza fedha nyingi katika elimu kwa kuboresha miundombinu na kuongeza walimu huku Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mapandepande Bi.Arodia Anatorya amesema ujenzi wa shule hiyo umesaidia kupunguza msongamano wa watoto katika shule ya Msingi Kiyombo ambayo hapo awali ilikuwa inakusanya wanafunzi wengi hali iliyochangia ufundishaji duni na utoro kwa baadhi ya wanafunzi tofauti na sasa ambapo ari ya kujifunza kwa wanafunzi imeongezeka na ufaulu ni mzuri.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa