Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe. Cornel Lucas Magembe amezindua chanjo ya mapele ngozi pamoja na zoezi la uogeshaji wa ng’ombe kwa kutumia dawa zinazotolewa kwa ruzuku. Zoezi hilo limefanyika leo katika kijiji cha Msuva,kata ya Ngoywa,wilayani Sikonge,ambapo zadi ya ng’ombe 200,000 wanatarajia kupatiwa chanjo hii muhimu ya mapele ngozi kufikia Julai 27,2024.
Akitoa taarifa ya hali ya chanjo ya mapele ngozi, Afisa mifugo wilaya ya Sikonge Dkt. Maulid Rajabu amesema kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/2023, Sikonge ilifanikiwa kuchanja ng’ombe 112, 116, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 ukilinganisha na idadi ya ng’ombe 99,303 waliopatiwa chanjo hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akihutubia wananchi na wafugaji waliojitokeza katika zoezi hilo,Mhe. Magembe ametoa rai kwa wafugaji kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa takwimu sahihi za mifugo yao ili serikali inapopanga mpango wa kuwahudumia wafugajiipange kulingana na mahitaji halisi katika kila eneo.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba sana wafugaji,unapokuwa umeambiwa utoe idadi sahihi ya ng’ombe ,si kwa nia nyingine ya kutaka kuwanyonya,la hasha,maana yake tunalenga tupate idadi sahihi ya ng’ombe mnaofuga,ili serikali ijue ni dawa kiasi gani inapaswa kuja katika eneo letu.” Ameeleza Mh. Magembe.
Ugonjwa wa mapele ngozi ni hatari kwa afya ya ngo’ombe ambao kwa kiingereza unafahamika kama Lumpy skin disease,ugonjwa huu kwa mara ya kwanza uligunduliwa nchini Zambia mwaka 1929,na kufikia mwaka 1989 ugonjwa wa mapele ngozi ulikuwa umeenea eneo zima la bara la Afrika na katika maeneo mengi ya bara la Asia na Kusini mashariki mwa bara la Ulaya.
Zoezi hili la utoaji wa chanjo ya mapele ngozi linaendeshwa na kampuni ya JEAA VETAGRO SOLUTION LTD, ambayo ndiyo iliyoshinda zabuni ya usambazi wa chanjo ya mapele ngozi wilayani Sikonge.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa