Mkuu wa Wilaya ya Sikonge,Mhe. Cornel Magembe ameongoza kikao cha kujadili utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa ngazi ya kata na wilaya kwa kipindi cha robo ya tatu katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge.
Akifungua kikao hicho Mhe. Magembe amewasihi wajumbe kuzingatia utekelezaji wa viashiria vyote vya lishe hususani utoaji wa chakula shuleni ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
Awali akitoa salamu za Halmashauri,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Bi. Kalista Maina amesema katika kipindi cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri imefanya shughuli mbalimbali za usimamizi na kuwezesha utekelezaji wa afua za lishe kwa ufanisi unaoridhisha na juhudi zinaendelea kufanyika ili kufanya vizuri zaidi ya katika kipindi kijacho.
Afisa Lishe Wilaya ya Sikonge Bi. Veronica Ferdinand amesema katika robo ya tatu siku ya afya ya lishe ya kijiji imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali wa kata wakiwemo maafisa kilimo,maafisa elimu pamoja na watoa huduma za afya ngazi ya kijiji,jambo hilo limeleta tija kubwa katika kuongeza elimu na uelewa wa masuala ya lishe katika jamii.
Akifunga kikao hicho Mhe. Magembe amepongeza utekelezaji mzuri wa shughuli mbalimbali za afua za lishe katika robo ya tatu hasa kwa kata zilizofanya vizuri zaidi ambazo ni kata ya Kisanga,Kipili na Igigwa vilevile ameelekeza apatiwe taarifa rasmi ya ukusanyaji,utunzaji pamoja na matumizi ya chakula shuleni ili kuondoa dosari za upotevu wa chakula hicho na kuondoa malalamiko yanayoelekezwa kwa wataalam katika ngazi ya shule na kata.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa