MAPAMBANO DHIDI YA VVU SIKONGE
Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI wilayani Sikonge mkoani Tabora yapungua kutoka asilimia 5.5% mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.2% mwaka 2018.
Takwimu hizo zilitolewa na mratibu wa UKIMWI ndugu Nicholas Magoha katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambapo wilayani Sikonge yalifanyikia katika kijiji cha Mlogolo na kubeba kaulimbiu ‘’JIPIME JITAMBUE ISHI”
Pia maadhimisho hayo yaliambatana na uchangiaji damu kwa hiyari ambapo jumla ya wananchi 18 walijitokeza kuchangia damu. Vilevile wananchi 213 ikiwemo wanafunzi wa shule ya msingi, pamoja na wazee walipima ili kujua afya zao, kati yao 3 waligundulika kuwa na VVU.
Katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi alikuwa Mhe. Peter Nzalalila Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, alitoa rai kwa sekta ya afya kuongeza vituo vya kuhudumia wagonjwa wa UKIMWI kutoka vituo 15 vilivyopo hadi kufikia vituo 35 ikiwa ni jumla ya vituo vya afya vilivyopo Sikonge.
Vilevile Mhe. Mwenyekiti alikemea unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa UKIMWI, na kusema ‘’ UKIMWI ni ugonjwa kama magonjwa mengine ni kwanini watumiaji wa ukimwi wamezee dawa chumbani?” aliwataka watumiaji wa dawa za VVU kuwa huru kutumia dawa zao bila kificho.
Aidha Mhe. Nzalalila alisisitiza kuepukana na ngono nzembe kwa kusema ‘’UKIMWI upo na UKIMWI bado tishio hivyo wanachi wajihadhari” na kuwataka wananchi wajiepushe na imani potofu kwa kukimbilia kwa waganga mara tatizo linapotokea. Pia waganga wa kienyeji waepuke kuchanja wagonjwa kwa kutumia wembe mmoja kwani ni chanzo kimoja wapo cha maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI.
Sanjari na hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Bi. Martha Luleka alisema ‘’ Afya ni mali na kama hauna Afya basi hauna mali.”
Mkurugenzi aliwasisitiza wana sikonge juu ya 90 tatu na kufafanua 90 ya kwanza ni kuhakikisha 90% ya watanzania na dunia nzima wawe wamepima na kujua afya zao ifikapo 2020. 90% ya pili ni waathirika wa ugonjwa UKIMWI wawe wameshaanza kutumia dawa za kupunguza maambukizi ya VVU na 90% ya tatu ni kuhakikisha waathirika wa UKIMWI waliopima na kuanza kutumia dawa za kupunguza makali wawe na uhakika wa maisha yao. Hivyo kuwataka wananchi wote wa Sikonge kupima na kujua afya zao ili waweze kuzilinda.
Maadhimisho hayo pia yaliambatana na vikundi mbalimbali vya burudani ambavyo vilikuwa na ujumbe uliotoa elimu juu ya ujongwa hatari wa UKIMWI. Pia katika michezo kulikuwa na mpira wa miguu na mpira wa pete ambapo timuya mpira wa miguu ya Sikonge iliibuka kidedea kwa kuinyuka magoli mawili timu ya Mlogolo.
Wananchi pia walipata nafasi ya kutoa pongezi zao kwa viongozi wilayani Sikonge na uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. Jonh Pombe Magufuli kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya Afya wilayani Sikonge na kutoa fedha kiasi cha Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, jambo litakalorahisisha utolewaji wa huduma ya afya.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA TEHAMA SIKONGE
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa