MADIWANI WASHUSHA NYUNDO KWA WAHUDUMU WA AFYA SIKONGE.
Wahudumu wa Afya Wilayani Sikonge waagizwa kuwa makini katika kutoa huduma kwa jamii inayowazunguka.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila katika baraza la Madiwani lililofanyika mapema jana kwenye ukumbi wa chuo cha ufundi kilichopo Sikonge, baada ya madiwani kutoa malalamiko ya wananchi kwa baadhi ya wahudumu wa Afya kutowatendea haki wagonjwa wanapofika katika vituo vya kutolea huduma hiyo.
Aidha, Mhe. Nzalalila alitoa onyo kali kwa watoa huduma za afya kuzingatia utaratibu wa kuwahudumia wagonjwa kwa upendo kwani ndivyo maadili yanavyowataka na waache kuwa na fikra za kuzani kuwa maelekezo wanayopewa ni siasa tu kwa sababu swala la Afya ni swala nyeti sana na ndio maana serikali imetoa pesa nyingi kuhudumia sekta hiyo.
“juzi tu serikali imeidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya dawa na huduma za Afya, lakini leo mgonjwa anafika hospitali anaambiwa kuwa hakuna dawa. Lugha hii ikome kwasababu hatutovumilia habari hii katika Wilaya yetu” alisema.
Hoja hii iliibuka baada ya Mhe. Upendo Mgombozi diwani Kata ya Kipanga kueleza namna ambavyo mwananchi wake aliyekuwa mjamzito kutopatiwa huduma stahiki huku akiambiwa kwenda kununua dawa katika zahanati ya jirani
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wakifatilia kwa makini mjadala unaoendelea kwenye vikao vya baraza.
Wajumbe walienda mbali zaidi na kuongeza kuwa kumekuwa na matukio mbalimbali ya wanawake wajawazito kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya na kurudishwa nyumbani kwa kigezo cha kuwa muda wao wa kujifungua haujafika, kitendo hiko kimepelekea baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani.
Akikemea kitendo hicho Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri alisema kuwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo hatovumiliwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. “tuliwahi kumuweka ndani muhudumu wa Afya hapa hapa Sikonge kwa vitendo hivyo , sitovumilia kuona mambo haya yanajirudia tena”.
Akijibu tuhuma hizo kaimu mganga mkuu wa Wilaya Theopista Elisa alisema kuwa kitaalamu hutokea mjamzito akawahi kujifungua tofauti na muda uliooneshwa kwenye vipimo ambapo hali hiyo ikitokea nesi anaweza kutumia majibu ya vipimo kumruhusu mama kurudi nyumbani hali hii inachangia kuwa sababu ya baadhi ya matukio kama hayo yakatokea.
Vile vile Dkt Theopista alihakikishia baraza kuwa anafanyia kazi jambo hilo na matukio yote ya unyanyapaa wa wagonjwa unaofanywa na watoa huduma wa afya ili kuzuia matukio kama hayo yasiweze kujitokeze tena Wilayani hapa huku akiwaomba madiwani na wananchi wote kutoa ushirikiano kwa kuwabainisha wale wote wanaohusika na malalamiko hayo ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa zidi yao.
Sanjari na jambo hilo pia baraza hilo pia walizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya barabara inayofanywa na Wakala wa Barabara vijijini na mjini TARURA ambapo kwa Sikonge imeonekana kufanya vizuri.
` IMEANDALIWA NA
KITENGO CHA TEKINOLOJIA HABARI NA MAWASILIANO TEHAMA
SIKONGE.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa