SIKONGE- MADIWANI WALIOPITA BILA KUPINGWA WAAPISHWA RASMI
Hakimu Wilayani Sikonge Mhe. Amando Nyami amewaapisha Madiwani hao wateule waliopita bila kupingwa katika uchaguzi mdogo mapema mwezi Juni 2019.
Madiwani hao ni Mhe. John Mbogo wa kata ya Ipole na Mhe. Josephine Mayanga wa kata ya Pangale wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliapishwa katika ukumbi wa chuo cha ufundi (FDC) mbele ya wajumbe wa kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, wataalamu wa Halmashauri, viongozi wa Chama Tawala CCM pamoja na Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Madiwani hao walipita bila kupingwa kufuatia wagombea wengine kutoka vyama pinzani kujitoa kwa hiari kushiriki uchaguzi baada ya kusema kuwa wanaimani na viongozi hao waliotokana na chama Tawala kuwa wataongoza vyema.
Aidha wakati wa kuapishwa kwa Madiwani hao Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sikonge, Marha Luleka alitoa pongezi zake kwa viongozi hao wapya huku akiahidi kufanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa.
Akizungumzaa kwa niaba ya chama, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mhe. Anna Chambala alitoa nasaha zake kwa wateule hao kuhakikisha kuwa wanatekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kuwatumikia wananchi wote bila kuwabagua kutokana na itikadi zao.
Wahe. Madiwani Wapya Wakiwa kwenye Picha ya pamoja na viongozi wa Halmashauri (waliokaa) pamoja na Whe. Madiwani kamati ya fedha mara baada ya kuapishwa mapema leo hii.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila aliwapokea kwa mikono miwili Madiwani hao huku akiwataka kuondoa woga wa kuchangia mawazo ya kimaendeleo kwani lengo ni kuwawakilisha vyema wananchi hususani katika swala la maendeleo, kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazowaongoza madiwani. Ili kusisitiza hilo Mhe. Nzalalila aliwakabidhi vitabu vya kanuni za Madiwani ili viwape muongozo sahihi.
Tume ya Uchaguzi ilitoa kibali cha kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kata ya Ipole baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo kupitia tiketi ya CHADEMA kujivua uwanachama na madaraka na kujiunga rasmi CCM ili kuonesha kuwa anakubaliana na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM sanjari na kuunga mkono utendaji kazi wa Mhe. John Pombe Magufuli Rais wa Tanzania.
Wakati Diwani wa Kata ya Pangale Mhe. Josephine ameingia madarakani baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo kufikwa na Mauti. Hivyo uchaguzi ulitangazwa na baada ya kukosekana upinzani mteule huyo alipitishwa bila kupingwa na leo hii wameapishwa rasmi tayari kuanza majukumu yao.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
TEHAMA SIKONGE
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa