MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI WILAYANI SIKONGE
Na.Anna Kapama,
Wilayani Sikonge maadhimisho ya siku ya wanawake ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8 mwezi Machi,yamefanyika katika viwanja vya TASAF kata ya Tutuo, huku Mgeni rasmi akiwa Katibu Tawala wa Wilaya, Renatus Mahimbali ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya. Katibu Tawala amewasisitiza wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi huku akiongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kike umeongezeka kuonesha kwamba wanawake wanaweza.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu WANAWAKE KATIKA UONGOZI;CHACHU KUFIKIA DUNIA YENYE USAWA yalianza kwa maandamano katika Shule ya Msingi Muungano hadi viwanja vya TASAF.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Susana Makoye aliyemuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, amewaomba wanawake kudumisha upendo katika familia hasa kuheshimu na kuwajibika katika majukumu yao,huku akisisitiza kusameheana ili umoja na mshikamano uweze kudumu katika familia.
Kwa upande wake Mhe.Juma Ikombola, Diwani Kata ya Misheni aliyemuwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya amewapongeza wanawake kwa kuwa wameonesha mchango mkubwa katika jamii na katika ngazi za uongozi, na kuongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge haiko nyuma katika kuwawezesha wanawake kwani imetenga fedha kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali kiasi cha Shilingi Milioni 120.
Nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Anna Chambala amewapongeza wanawake kwa kusema mwanamke ni mlezi wa familia, huku akiipongeza Serikali kwa kuwapa nafasi katika uongozi na kuwataka wanawake kushikamana ili kuleta maendeleo endelevu.
Maadhimisho hayo yameambatana na huduma mbalimbali ikiwemo uchangiaji damu pamoja na Elimu ya afya ya Uzazi ambapo wananchi wamejitokeza kuchangia damu na kupata Elimu hiyo ya Afya ya Uzazi.
Historia fupi ya siku ya wanawake duniani ;Waanzilishi wakuu wa siku hii kilikuwa ni chama cha kijamaa kutoka nchini Marekani kikiongozwa na mwanamke Clara Zetkin ambae alipendekeza wazo hilo katika mkutano wa wanawake uliofanyika mnamo Februari mwaka 1908 huko COPENHAGEN Nchini Denmark na kuhudhuriwa na wanawake kutoka mataifa mbalimbali Duniani.
Kwa mara ya kwanza siku ya wanawake Duniani ilisherehekewa mnamo mwaka 1911 katika mataifa ya Denmark,Australia,Switzerland na Ujerumani ikiwa haijapitishwa rasmi na umoja wa mataifa, na baadae mnamo mwaka 1975 ikapitishwa rasmi na Umoja wa Mataifa kuwa siku ya wanawake Duniani kila ifikapo tarehe 8 mwezi Machi.(source,bbc)
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa