MAADHIMISHO YA SERIKALI ZA MITAA SIKONGE
Sherehe za maadhimisho ya Serikali za mitaa hufanyika Julai Mosi ya kila Mwaka. Serikali za mitaa inajumuisha uongozi kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata hadi Wilaya.
Maadhimisho hayo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge yamefanyika katika Kata ya Nyahua kijiji cha Makibo jana. Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Peter Mihayo Nzalalila.
Aidha, mgeni rasmi aliambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Paschal Ngunda ambaye pia aliambatana na Wakuu wa Idara.
Akimkaribisha mgeni rasmi Mwenyekiti wa Kijiji cha Makibo, Ndogosa lubinza alifurahi sana kwa ujio wa ugeni huu kwa ajili ya maadhimisho hayo na aliwakaribisha sana katika kijiji cha Makibo.
Mheshimiwa diwani wa kata ya Nyahua, Andrea Masanja nae aliwakaribisha Wageni na kutoa changamoto zinazoikabili kata yake ambazo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. " Kata yangu inachangamoto kubwa mbili, kwanza miundombinu ya barabara ni mibovu inakwamisha huduma za kijamii kama afya na shule lakini pia mawasiliano ya mitandao ambayo inatuwezesha kuwasiliana na kutoa taarifa hasa za matukio ya dharua ni shida sana" alizungumza kwa uchungu sana diwani huyo.
Aidha, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Mrishi ambae pia ni mlezi wa kata hiyo aliwaasa wananchi na kuwataka kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ili kuijenga Kata yao kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mgeni rasmi alizungumzia na kusisitiza juu ya majukumu ya viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji na kuanza kuwauliza baadhi ya viongozi kama wanayafahamu majukumu yao. Viongozi wengi waliosimamishwa na mgeni rasmi kutaja majukumu yao walifanya vizuri na aliwasifu sana kwa kutambua majukumu yao.
Aidha, mgeni rasmi aliwaasa wafugaji kutoshawishika kutoa rushwa kwa hali yoyote ile na pia viongozi wajiepushe na suala la rushwa na wajikite katika kutoa huduma kwa jamii kwa kufuata taratibu na kanuni. “ Wananchi huduma zote ngazi ya kitongoji hadi kata ni bure, msitowe hela yoyote…” alisema mgeni rasmi.
Pia mgeni rasmi alisisitiza suala la kuwapeleka shule watoto wote wenye umri wa kwenda shule na alisisitiza kuwalinda, kuwajali watoto hasa wa kike. Aliwataka viongozi na walimu kukomesha utoro wa wanafunzi na mimba za utotoni na kukumbushia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri ambae aliagiza kuwepo kwa maandamano siku ya Julai 2 katika kila kata yenye kauli mbiu ya “Oparesheni Kamata Weka Ndani kwa Kutotii Amri Halali”.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa