Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Kamagi, huku lengo likiwa kutoa elimu juu ya umuhimu wa lishe bora kwa vijana.
Akifungua maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Bi. Kalista Maina, amewasisitiza wanafunzi kuzingatia mlo kamili wa vyakula kutoka makundi sita muhimu, ikiwa ni pamoja na vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde,vyakula vya asili ya nafaka,mizizi na ndizi mbichi,vyakula vya sukari,mafuta na asali,matunda na mbogamboga.
Bi. Maina ameogenza kuwa ni muhimu kwa vijana kuanzisha ulimaji wa mbogamboga na upandaji wa miti ya matunda ili waweze kupata vyakula mchanganyiko vinavyohitajika kwa afya bora.
Aidha, Afisa Lishe Wilaya ya Sikonge, Bi. Veronica Ferdinand, amesisitiza kuwa ulaji bora ni muhimu kwa ukuaji wa vijana, akisema kuwa wanahitaji nishati bora ili waweze kujifunza kwa ufanisi.
Maadhimisho hayo yamejumuisha burudani mbalimbali, kama maigizo, ngojera, na maonesho ya mabango kuhusu lishe, yakitilia mkazo kauli mbiu ya mwaka huu isemayo : “Mchongo ni afya yako, zingatia unachokula.” Katika maadhimisho hayo, jamii ya shule, pamoja na walimu, wamehudhuria kwa wingi, wakionesha umuhimu wa kujifunza kuhusu lishe bora kwa ajili ya afya zao.
Lengo la maadhimisho haya ni kufikia vijana na kuimarisha uelewa wao kuhusu mapendekezo ya mwongozo wa kitaifa wa chakula na ulaji.Maadhimisho hayo yamefikia tamati Oktoba 30, 2024 nchi nzima.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa