KIKAO CHA KAMATI YA AFYA YA MSINGI WILAYA YA SIKONGE CHAFANYIKA KUJADILI MPANGO MKAKATI KUHARAKISHA KASI YA UTOAJI CHANJO YA UVIKO-19.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.John Palingo ameongoza kikao cha Kamati ya Afya ya kilichofanyika Leo 22/9/2021 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Akifungua kikao,Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Palingo amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujadili namna ya kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo ili kuongeza kasi ya watu kupata chanjo hiyo ya UVIKO-19.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa chanjo katika Wilaya hiyo,Mratibu wa huduma za Chanjo(W) Muku Masoud amesema Wilaya ya Sikonge ilipokea dozi 3,710 ya chanjo ya "Janssen" mnamo Agosti 4,2021 ,lakini mpaka kufikia Septemba 21,2021 jumla ya waliopata chanjo hiyo ni watu 342 sawa na asilimia 9.2 tu.
Aidha,Masoud amesema kumekuwa na muitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupata Chanjo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo wa wananchi juu ya umuhimu wa chanjo,wahudumu wa chanjo kutokupatiwa mafunzo ya chanjo ya UVIKO-19,Viongozi wa Siasa,Dini na Watu mashuhuri kutopatiwa uelewa wa kutosha kuhusu Chanjo hiyo ili wasaidie kuhamasisha jamii.Kamati hiyo imejadili mikakati inayotarajiwa kutekelezwa ili kuharakisha kasi ya utoaji chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi katika Wilaya ya Sikonge ikiwemo kuongeza vituo na kusambaza chanjo katika vituo vyote 36 vya kutolea huduma za Afya, kufanya huduma ya mkoba kwa maeneo yaliyo mbali na vituo vya chanjo na sehemu zenye mikutano ya hadhara,minada, na vyuoni,na pia kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya chanjo.
Kwa upande wake Afisa kutoka Wizara ya Afya ,maendeleo ya jamii,Jinsia Wazee na watoto Dr.Yahaya Hussein amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya watoa huduma ya Chanjo ili kurahisisha huduma hiyo.
Utekelezaji wa Mikakati hiyo unatarajiwa kuongeza kasi ya uchanjaji wa UVIKO-19 ifikapo Oktoba 15,2021.
Na.Anna Kapama
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa