Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mhe. Rashid Maulid Magope, ameongoza kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne, ambapo amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na weledi katika utendaji kazi. Katika kikao hicho, Mhe. Magope ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri kuendelea kutimiza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa na kutoa ushauri wa kitaalam kwa waheshimiwa madiwani ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wa makusanyo ya mapato, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imepata mafanikio makubwa, ikikusanya shilingi bilioni 3.9 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, sawa na asilimia 97.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5% ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Sikonge, Mhe. Anna Wilson Chambala, amelipongeza baraza hilo kwa kuendesha kikao kwa weledi na utulivu, akisema, “Nimefurahishwa sana na jinsi kikao kilivyoendeshwa, haya ndio tunayoyataka sisi CCM.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Seleman Pandawe, ametoa wito kwa madiwani kuelimisha umma kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, huku akihimiza wananchi kujiandikisha kuwa wapiga kura na kugombea nafasi za uongozi.
Katibu Tawala wa Wilaya, Ndg. Andrea Ng’hwani, amefikisha maagizo ya mkuu wa wilaya mbele ya baraza la madiwani kuhusu umuhimu wa kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafikia asilimia mia moja na usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Katika kufunga kikao hicho, Mhe. Magope amerudia mwito wake kuhusu uwajibikaji na weledi, akisisitiza kwamba hiyo ndiyo njia bora ya kuharakisha maendeleo katika wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa