Na. Robert Magaka – Sikonge.
Katibu Tawala Wilaya ya Sikonge Ndg. Andrea Ng'hwani ametembelea shule tano za sekondari kufuatilia mwitikio wa mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2024, katika ziara hiyo Ng’hwani ameambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sikonge Bi. Kalista Maina pamoja na Afisa Tarafa ya Sikonge Bi. Faraja Hebel.
Shule alizotembelea ni pamoja na Ugunda Sekondari,Chabutwa,Kamagi,Shule mpya ya Sikonge Sekondari pamoja na Shule ya Sekondari Mkolye.
Akizungumza mbele ya walimu pamoja na Wajumbe wa baraza la kata ya Ipole Ndg. Ng’hwani amesema mahudhurio sio mazuri ukilinganisha na uhalisia wa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari kwa mwaka 2024, hivyo amewataka Viongozi wa Kata pamoja na walimu kushirikiana na Wazazi kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari wanaripoti mara moja ili kuendelea na masomo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi amewapongeza Walimu wa Shule ya Sekondari Ugunda kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha pili 2023 kwa kupata ufaulu wa asilimia 85% na kuwasihi kuzidisha juhudi katika kuondoa kabisa Daraja la nne katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Akihitimisha ziara hiyo Katika Shule ya Sekondari Mkolye Katibu Tawala Wilaya ya Sikonge ametoa wito kwa wazazi na walimu kuwasisitiza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na bado hawajafika kuripoti shuleni haraka hata kama hawajakamilisha mahitaji ya msingi zikiwemo sare za shule na mahitaji mengineyo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa