Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Cornel Lucas Magembe ameongoza kamati ya usalama kukagua miradi itakayopitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
Katika ziara hiyo kamati ya Usalama imekagua mradi wa ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika shule ya sekondari Kiwere yenye thamani ya shilingi milioni 234, mradi unaendelea vizuri upo katika hatua za upauaji.
Mhe. Magembe amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Seleman Pandawe,Diwani wa Kata ya Kitunda Mhe. Ismail Mnakwanza pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiwere Mwl. Bakari Nahoda pamoja na kamati ya ujenzi wa mradi huo kwa utekelezaji wa mradi huo kwa viwango vinavyoridhisha. “Kwa kweli nawapongeza kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea nayo ,kwa hiyo mimi nikupongeze sana mheshimiwa diwani,mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata lakini na watendaji wako kwa jinsi walivyosimamia,lakini mwalimu na wewe tukupongeze kwa sababu wewe ndio mradi upo kwako ukicheza vibaya mradi unaharibika,nimefurahi ukiangalia hata fisherboard ilivyopigwa,ukweli ubao umenyooka sawasawa inavutia kutazama hata kwa mbali, nawapongeza sana kwa kweli.”amesema Mhe. Magembe.
Mradi mwingine uliokaguliwa ni ujenzi wa mradi wa maji,mtandao wa ziwa Victoria kwenda miji ya Sikonge,Urambo na Kaliua,mradi huu unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 40.9 mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba kuu la usafirishaji maji kutoka bomba kuu la maji ya ziwa Victoria kuja Tabora Mjini na kuelekea mji wa Sikonge pamoja na ujenzi wa matanki mawili ya maji safi,ujenzi umefikia asilimia 19%.Baada ya ujenzi kukamilika jumla ya vijiji 23 na wananchi 164,766 pamoja na mifugo watanufaika na huduma ya maji safi na salama.
Kamati ya usalama umeridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo,wameshauri kasi ya ujenzi iendelee pamoja na kuhakikisha nyaraka zote za ujenzi ziandaliwe na kutunzwa vizuri na kuhakikisha wazabuni wa miradi hii wanalipwa kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa