Na Edigar Nkilabo.
hKamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Sikonge imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyopendekezwa kutembelewa,kuwekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2025 ambao unaotarajiwa kupokelewa Wilayani Sikonge mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza katika ziara hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Katibu Tawala wa Wilaya Sikonge Andrea Ng’hwani amewataka wataalamu na wasimamizi wa miradi inayotekelezwa Wilayani Sikonge kuhakikisha taratibu zote za manunuzi zinazingatiwa na miradi inakamilika kwa wakati ikiwa na ubora unaokidhi viwango vya kitalaamu ili Mwenge wa Uhuru utakapopita basi miradi hiyo iweze kuzinduliwa,kukaguliwa na kuwekewa jiwe la msingi.
Aidha Katibu Tawala Ng’hwani amemtaka Mhandisi wa Wilaya kufuatilia nyaraka zote za vipimo vya malighafi za ujenzi ikiwemo nondo,zege na mabati ili kuwa na uhakika wa shughuli zote za ujenzi wa miradi ya maendeleo itakayopitiwa na mwenge.
“Hakikisheni nyaraka zote zinapatikana kwa wakati msisubiri Mwenge ukaribie ndiyo muanze kufukuzana kuzitafuta hizo nyaraka tena ikiwezekana zipatikane mapema kabla hata kamati ya mkoa hijaja kuikagua hii miradi”amesema.
Kwaupande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Nico Kayange amesema changamoto zote zilizotolewa na amezipokea na atakaa na wataalamu wanaohusika ili kuzipatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama imepita kukagua miradi ya Afya, elimu na vikundi vya wajasiriamali katika kata za Sikonge,Tutuo na Misheni.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa