Na. Robert Magaka – Sikonge.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Juma Nkumba, ameiongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM (2020-2025) wilayani Sikonge, mkoani Tabora. Katika ziara hiyo, kamati hiyo ilikagua miradi miwili ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha kutoka serikali kuu pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa njia za kupitia wagonjwa (walkway) katika hospitali ya wilaya ya Sikonge, ambapo ujenzi huo unafanyika kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, na unagharimu jumla ya shilingi milioni 100. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 80. Aidha, kamati hiyo pia ilikagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu kumi ya vyoo katika shule ya sekondari Sikonge. Ujenzi huu unafanyika kwa fedha kutoka serikali kuu na umegharimu shilingi milioni 398, na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 50.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Ndg. Nkumba ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi yote miwili na kutoa wito kwa wananchi wa Sikonge kuendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza juhudi za kujitolea nguvu kazi katika maeneo ambako miradi hiyo inatekelezwa.
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Sikonge, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Ndg. Anna Wilson Chambala, wametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambayo inatekelezwa wilayani Sikonge na maeneo mengine nchini. Viongozi hao waliahidi kuendelea kuunga mkono serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kutimiza malengo ya maendeleo.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tabora inaendelea na ziara ya siku mbili kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya mbalimbali za mkoa huu. Ziara hiyo inatarajiwa kumalizika kesho, Desemba 19, kwa kutembelea halmashauri za wilaya ya Igunga, Nzega, Nzega Mji pamoja na Uyui.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa