Mhe. Rashid Magope ameongoza wajumbe wa kamati ya fedha,uongozi na mipango kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Kamati hiyo imefanya ukaguzi katika mradi wa ukarabati wa jengo la maenesho ya nanenane lililopo kata ya Ipuli katika manispaa ya Tabora linalogharimu kiasi cha shilingi milioni 18,likihusisha kuziba nyufa,kuweka dari,kupaka rangi ,kusuka nyaya za umeme,kukarabati wa milango,kukarabati mfumo wa maji taka pamoja na kuweka wavu kwenye madirisha,hatua ya mradi imefikia asilimia 40% ya utekelezaji wake.
Vilevile kamati hii imezuru mradi wa ujenzi wa jengo la kufulia katika kituo cha afya Kiyombo kilichopo kata ya Kipili unaogharimu shilingi milioni 35.9.Mradi umefikia asilimia 80% na upo hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mradi mwingine uliokaguliwa ni ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika shule ya sekondari Kiwere iliyopo kata ya Kitunda wenye gharama ya shilingi milioni 234, ujenzi umefikia asilimia 60% ya utekelezaji na mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2024 mradi huu utakuwa umekamilika.
Wakiwasilisha ushauri na maoni wajumbe wa kamati hii wamesema dosari zote zilizobainika katika hatua mbalimbali za utekelezaji zirekebishwe na wamemwagiza mhandisi wa ujenzi wilaya ya Sikonge kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa yafanyiwe kazi ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Seleman Pandawe amewasihi wote waliokasimishwa madaraka kwa niaba ya mkurugenzi wahakikishe wanatimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kufuata maagizo yote yanayotolewa na Serikali hususani suala nzima la kuzingatia ununuzi wa umma ufanyike kwa njia ya mfumo wa NeST na wala si vinginevyo.
Akihitimisha ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Rashid Magope amesisitiza kuongeza jitihada na kasi ya ujenzi kwa kuzingatia ubora na umaridadi wa kazi, kwani miradi hiyo inatarajiwa kuja kuzinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa