Na Edigar Nkilabo – SikongeDC
Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata tofauti ndani ya Halmashauri ikiwemo miradi ya Elimu,Afya,Utawala na Mazingira ambapo Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Ndg.Gastor A. Rwambano imekiri kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo iliyoanza tarehe 26 Januari, 2026, kwa kamati kutembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati Kiloleli wenye thamani ya shilingi 250,000,000/= fedha za serikali kuu na shilingi 9,000,000/= za nguvu ya Wananchi ikiwemo usafishaji wa eneo,kubeba mchanga,mawe pamoja na fedha taslimu.
“Tumefurahi kuona mradi huu unaendelea licha ya changamoto zilizokuwa nje ya uwezo wenu Wataalam wetu lakini kazi inaonekana na hapa tungeshauri mafundi waongezwe ili kasi iongezeke mradi ukamilike kwa wakati”alisema Mwenyekiti wa Kamati Ndg.Gastor Rwambano.
Aidha Kamati hiyo imekagua mradi wa elimu ujenzi wa vyumba 03 vya madarasa na matundu 06 ya vyoo kwa shule ya Msingi pamoja na vyumba 02 vya madarasa ya Awali na matundu 06 ya vyoo kwa fedha za BOOST shilingi 160,000,000/= ambapo baadhi ya vyumba tayari vimekamilika na vingine vikiendelea kujengwa.
Miradi mingine iliyokaguliwa na Kamati ni ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambapo Kamati iliidhinisha zaidi ya shilingi 50,000,000/= za mapato ya ndani kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ambayo imejengwa kwa fedha za serikali kuu na mapato ya ndani kwa awamu tofauti kuanzia mwaka 2012. Pia kitalu cha miche ya matunda cha Halmashauri kimekaguliwa na Kamati pamoja na Hospitali ya Wilaya Mlogolo ambapo wamekagua njia za kuunganisha majengo 9Walkways) mradi ambao umetekelezwa kwa awamu mbili kwa mapato ya ndani shilingi milioni 120 na milioni 41 za serikali kuu hadi kukamilika kwa njia hizo.
Baada ya kukagua miradi hiyo ikiwemo jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya, Kamati imeipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na kusisitiza wataalam kufanyia kazi maelekezo ya kamati ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuanza kuwanufaisha Wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa