HALMASHAURI YA WILAYA YA SIKONGE YAKAMILISHA UJENZI WA KITUO CHA REDIO JAMII (SIKONGE FM) KWA SHILINGI 190,455,100/= ZINAZOTOKANA NA MAPATO YA NDANI
Na, Edigar Nkilabo – SikongeDC
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imekamilisha mradi wa ujenzi wa Kituo cha Redio chenye masafa ya 98.9 Sikonge FM – Sauti ya Nyuki kwa fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri lengo ikiwa ni kuwahabarisha , kuwaelimisha na kuwaburudisha Wananchi wa Wilaya ya Sikonge na maeneo ya jirani.
Akizungumza katika Kituo hicho kilichopo kata ya Sikonge, wakati wa Ziara ya Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango (FUM), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg.Selemani Pandawe amesema Halmashauri imetumia zaidi ya shilingi milioni 190 kwaajili ya mradi wa kituo hicho ili kuhakikisha kila Mwananchi anapata habari ya masuala ya maendeleo yanayotekelezwa na serikali pamoja na taarifa mbalimbali za fursa za kiuchumi.
Aidha Pandawe amesema mradi huo umeanza kwa usikivu unaofikia umbali wa Kilomita 120 lakini kwa siku za mbeleni Halmashauri itaongeza umbali wa usikivu na kuwafikia watu wa tarafa ya Kiwere ambao kwasasa hawaipati redio hiyo.
“Kutokana na Jiografia yetu ya Sikonge eneo ni kubwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kuna umbali mrefu hivyo tunaamini kupitia matangazo mbashara ya redio Wananchi wetu watapata taarifa kwa haraka na elimu ya masuala ya kijamii,kiraia na kiuchumi itawafikia haraka na kuwaongezea uelewa wa kampeni mbalimbali za serikali katika nyanja zote ”alisema Ndugu Selemani Pandawe.
Naye Mjumbe wa FUM, Mhe.Christina Singiwa amesisitiza kuongezwa kwa masafa ya usikivu wa matangazo ya redio ili isiishie kusikika tarafa ya Sikonge bali hadi tarafa ya Kiwere Wananchi wanaoishi kata za Kitunda,Kiloli,Kilumbi na Kipili waweze kuyapata mawimbi ya redio Sikonge.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Kamati ya FUM, Mhe.Gastor Rwambano amesema kamati yake imeridhishwa na mradi huo na kuwataka wasimamizi wa mradi kukamilisha kwa haraka matengenezo madogo madogo yaliyosalia ili kituo hicho kianze kufanya kazi na kuwahudumia Wananchi.
“Kwa niaba ya Kamati niseme tumefurahi na tumeridhishwa na maendeleo ya mradi huu lakini tunaelekeza marekebisho yaliyosalia yafanyike kwa haraka ili wenye Mamlaka (TCRA) waje kukagua kituo chetu waturuhusu ili tuanze kupasua anga “alisema Mhe.Gastor Rwambano.
Kamati hiyo imetoa wito kwa Wasimamizi wa Kituo hicho na Wataalam kuchakata gharama za huduma ya matangazo kwa kuzingatia ukubwa wa bidhaa husika au jambo lenyewe linalotakiwa kutangazwa.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa