Na, Edigar Nkilabo
Halmashauri ya wilaya ya Sikonge imetoa mikopo isiyo na riba ya shilingi 460,499,999 kwa vikundi 55 vya vijana, wanawake na wenye ulemavu ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za serikali ya awamu ya sita ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kupitia 10 % ya mapato ya ndani yanayotengwa kwa ajili ya kuinua kipato cha makundi hayo.
Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa utoaji mikopo isiyo na rib ani Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe.Cornel Lucas Magembe ambaye anaipongeza halmashauri ya wilaya ya Sikonge kwa kuendelea kutekeleza ilani ya chama na takwa la kisheria la kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya vijana ,wanawake na wenye ulemavu.
“Fedha hizi ni nyingi halmashauri mmetimiza wajibu wenu nitoe rai kwa vikundi vyote 55 ambavyo vimebahatika kupata mikopo hii isiyo na riba viende vikaanzishe biashara na kuendeleza miradi kama walivyoeleza katika maandiko waliyowasilisha wakati wa maombi ya mkopo ili waweze kujikwamua kiuchumi,kuongeza pato la taifa bila kupata tabu ya mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa ikiwaumiza wananchi wengi” Mhe.Magembe.
Aidha mkuu wa wilaya Mhe.Magembe amevitaka vikundi vyote vilivyokopa kurejesha fedha za mikopo hiyo kwa wakati kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa kuweza kutoa fursa kwa vikundi vingine kuomba na kupata fedha hizo ili kutimiza lengo la serikali la kuwawezesha wananchi wote wenye uhitaji kujiendeleza kiuchumi.
Kwa upande wao Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Tito Ruchagula na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mhe.Rashid Magope wamesema serikali imeandaa utaratibu mzuri ambao utasaidia mikopo kurejeshwa kikamilifu huku Katibu wa CCM Wilaya ya Sikonge Ndg.Salum Mgaya akieleza kukoshwa na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ambayo inaelekeza serikali kutenga fedha na kuwawezesha wananchi mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hii wanasema fedha hizo zitatumika kubadilisha hali zao za kiuchumi.“Fedha hizi zitanisaidia kuendeleza biashara zetu ambazo zinatupatia fedha ya kujikimu, ninasomesha watoto na kuwapatia mahitaji ya muhimu kwakweli ninaishukuru serikali ya awamu ya sita” Amina Ntalamba.
Jumla ya vikundi 107 viliomba mkopo wa asilimia 10 % usio na riba huku vikundi 55 pekee vikikidhi vigezo vya kupatiwa mikopo hiyo ambayo itaendelea kutolewa katika dirisha la pili.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa