Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe. Cornel Magembe ametembelea ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mwamayunga.Katika ziara hiyo Mhe. Magembe ameambatana na kamati ya Usalama wilaya,Wakuu wa taasisi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi,Meneja wa RUWASA-Sikonge ,Mhandisi Fikiri Samadi amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 70% ya utekelezaji na mradi utakapokamilika utakwenda kuhudumia wakazi 9,437 wa vijiji vya Mwamayunga,Isanjandugu,Usunga na Urafiki.
Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za PforR,unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.8 na mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimekwisha tumika katika mradi huo na kiasi cha shilingi bilioni 1.3 zimebakia kwa ajili ya kukamilisha asilimia 30% ya kazi zilizobakia.
Aidha mradi huu unahusisha uchimbaji wa mitaro na kulaza mabomba kwa umbali wa kilomita 33.2 kuvifikia vijiji vinavyokwenda kunufaika na mradi huu,ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita za ujazo 300M3,ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji,ujenzi wa ofisi moja ya jumuiya ya watumiaji maji ngazi ya jamii,ujenzi wa nyumba moja ya mitambo pamoja na ujenzi wa nyumba ya muendesha mitambo.
Mhe. Magembe amemwagiza mkandarasi wa mradi huo PALEMON CONSTRUCTION CO. LTD kufanya kazi kwa bidii na kwa haraka ili mradi ukamilike kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi wa wa kijiji cha Mwamayunga. “Sisi tukupe mpaka tarehe 30/05/2024 uwe umekamilisha mradi huu,Meneja simamia kazi ifanyike kwa kiwango sio kwa kulipua.”amesema Mhe. Magembe.
Mradi huu utakapo kamilika utakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma endelevu ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji Mwamayunga,kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama pamoja na kuwapunguzia adha ya kutafuta maji kwa umbali mrefu hivyo kuwaongezea muda wa kufanya shughuli zingine za kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa