Na. Robert Magaka – Sikonge.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Simon Chacha amezindua zoezi la utoaji wa chanjo ya Surua Rubella katika Hospitali ya Misheni iliyopo kata ya Misheni Wilayani Sikonge.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Chacha ametoa wito kwa wazazi na walezi kuitikia wito wa Serikali wa kuwapeleka Watoto wenye miezi 9 hadi miezi 59 kupata chanjo ya surua rubella katika vituo vya afya vilivyokaribu nao.
“Nawashukuru wazazi mliofika hapa natumaini mtakwenda kuhamasisha wazazi wengine kuwapeleka Watoto wao kupata chanjo ya surua rubella.Tafiti zimethibitisha kuwa Chanjo imeweza kuzuia vifo vya watu milioni 3 kila mwaka,kwa mfano kupitia chanjo tumeweza kutokomeza kabisa ugonjwa wa pepopunda,Ndui na Ugonjwa wa kupooza (Polio).” Amesema Mhe. Chacha.
Akitoa Salamu za Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Christopher Nyalu amesema katika zoezi hili Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imelenga kuchanja watoto 4,3281.
Naye Mwakilishi toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi. Nyabawela Ester Mahuyu amesema lengo la nchi ni kufikia Watoto 8,908,810 na Lengo la Mkoa ni kufikia Watoto 544,616 ili kupambana na ugonjwa wa surua rubella kwa ufanisi wananchi wanapaswa kuitikia wito wa Serikali kwa kuwapeleka Watoto katika vituo vya afya vilivyopo karibu ili wapatiwe chanjo.
Zoezi hilo limezinduliwa kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya kukata utepe na kushuhudia zoezi halisi kwa Watoto kupatiwa chanjo ya surua rubella,zoezi hili linaendelea katika maeneo yote vilipo vituo vya afya na zahanati na maeneo mengine yalitengwa mahususi kwa ajili ya zoezi hili.
Tanzania bila Surua inawezekana! Onesha Upendo Peleka Mtoto akapate Chanjo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa