Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe. Cornel Magembe ameongoza zoezi la uzinduzi wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi lililofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mbirani.
Mhe. Magembe ametoa wito kwa wananchi kuitikia chanjo hii hususani kwa walengwa ambao ni wasichana wenye umri kuanzia miaka 9 hadi 14 ili kuiepusha jamii na ugonjwa hatari wa saratani ya mlango wa kizazi ambao huwapata akinamama wengi nchini.“Ninawaomba sana muipokee chanjo hii,unapopata chanjo hii unakuwa na uhakika wa kutopata saratani ya mlango wa kizazi,lakini pia tunaliepusha taifa kuwa na wagonjwa wengi wa kansa hivyo kuiepusha serikali kughalamika kununua dawa za kutibu kansa.”amesema Mhe. Magembe.
Kwa upande wake mkuu wa divisheni ya afya,ustawi wa jamii na lishe Dkt. Christopher Nyalu amesema zoezi hili linalenga wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 ili kuwakinga na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi,Dkt.Nyalu ametoa wito kwa jamii kuitikia zoezi hili kwa usalama wa kizazi cha taifa,ameongeza kuwa wilaya ya Sikonge inatarajia kuwapatia chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi wasichana 30,307 na kwa kituo cha shule ya msingi Mbirani wanatarajia kuchanja wasichana 396 kufikia Aprili 24,2024, na zoezi hili linaloongozwa na kauli mbiu isemayo “Jamiii liyopata chanjo,Jamii yenye Afya” litaendelea kutolewa katika vituo vyote vya afya na zahanati.
Akitoa salamu na kufunga uzinduzi huo, diwani wa kata ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Sikonge kwa kuchagua kata ya Sikonge kufanyia zoezi hili la uzinduzi wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa juhudi hizi kubwa za kughalamia chanjo hii ambayo ni ghali na kuileta kwa wananchi bila ghalama yoyote.
Saratani ya mlango wa kizazi inasababishwa na virusi vya HPV (Human papilloma virus),mpaka sasa zimekwisha ripotiwa kesi 660000 za wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi duniani kote na saratani hii imekwisha sababisha vifo 350000 duniani kote kufikia mwaka 2022,ugonjwa huu huwaathiri wanawake pekee na wala hauna tiba mahususi isipokuwa unayokinga mahususi inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani bure.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa