BENKI KUU YA TANZANIA (BOT) WATOA ELIMU WILAYANI SIKONGE KUHUSU NOTI ZA TANZANIA
Tarehe 12.5.2021
_Na. Anna Kapama_ - Sikonge
Wakizungumza na wananchi katika kitongoji cha madukani maafisa hao wa BOT wametoa elimu hiyo ikiwa ni pamoja na alama zinazopatikana katika noti za Tanzania kutokana na uwepo wa watu wanaotengeneza noti bandia.
Meneja msaidizi Idara ya Uhusiano Vicky Msina amesema ni muhimu kwa wananchi kutambua alama muhimu zinazopatikana katika noti halali za Tanzania ili kuepuka utapeli wa kupewa noti za bandia hasa katika kipindi hiki cha ununuaji na uuzaji wa mazao na mifugo kutoka kwa wakulima na wafugaji.
Msina ameongeza kuwa ni vema kwa wafanya biashara kuwa na vifaa vinavyoweza kutambua noti halali na bandia ambavyo ni pamoja na taa maalumu zenye mwanga wa zambarau (ultraviolet light bulb) kwa kuwa taa hizo zina uwezo wa kutambua alama muhimu zilizo katika noti halali ambazo si rahisi kuzibaini kwa macho ya binadamu pasipo vifaa hivyo.
Kwa upande wake Lilian Silaa ambae ni mmoja wa waliotoa Elimu hiyo amewataka wananchi wa Sikonge kutoa taarifa katika vyombo vya usalama au kwa viongozi walio katika Serikali za mitaa mara wanapobaini kuwa wana noti hizo ili kuepuka mkono wa sheria wanapobainika. Lakini pia amewaasa wananchi wa Sikonge hasa wafanya biashara wakubwa na wauzaji wa mazao kutopendelea kupokea fedha taslimu mkononi badala yake watumie njia ya benki na huduma zingine za kifedha kama Airtel money,Tigopesa,M-pesa na zingine ili kuepuka kuchomekewa noti za bandia lakini pia kuepuka hatari ya kuporwa fedha zao.
Katika upande wa utunzaji wa noti za Tanzania watumishi hao wamewashauri wananchi kuzingatia utunzaji wa noti hizo kwa kuepuka kuzishika katika hali ya unyevu,kuzikunjakunja maana kwa kuzitunza zitaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi na kuepuka hasara ambazo Tanzania hupata kutokana kuwapo kwa noti nyingi chakavu zisizoweza kutumika tena.
Maafisa hao wa BOT wameendelea kutoa elimu kwa maeneo mbalimbali katika mikoa yote ya Tanzania ikiwa ni miongoni mwa majukumu yao kwa Umma.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa