Na, Edigar Nkilabo.
Baraza la Wafanyakazi Halmashauri ya wilaya ya Sikonge limepitia na kupitisha mapendekezo ya Katibu na Katibu msaidizi na kupiga kura za kuwathibitisha viongozi hao wapya ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu katika baraza hilo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha kuzindua mkataba wa Baraza la wafanyakazi Mwenyekiti wa Baraza hilo Seleman Pandawe amewataka viongozi waliopitishwa kuendeleza utamaduni wa kusimamia miiko na maadili ya wafanyakazi ili kuepusha migogoro na mizengwe mahali pakazi.
“Mmeaminiwa mmepata hii nafasi muende mkasimamie maadili ya wafanyakazi na kuwasikiliza ili mahali pa kazi pawe salama kila mfanyakazi afurahie mazingira ya kazi na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kama serikal inavyokusudia”amesema.
Afisa Kazi mkoa wa Tabora Muhenga Richard amesema vyama vya wafanyakazi vilianzishwa kwa lengo la kufikisha changamoto za watumishi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi ili wafanyakazi watimize wajibu wao katika mazingira mazuri na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la wafanyakazi Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Richard Msimu amewashukuru wajumbe wa Baraza hilo kwa kumpa ridhaa yeye na Katibu msaidizi Mary Ruley na kuahidi kuwa watatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maoni na matakwa ya baraza la wafanyakazi.
“Tunashukuru kwa kutuchagua ninawahakikishia tutafanya kazi kwa karibu nanyi kwa kuzingatia maoni na ushauri wenu ili tusonge mbele kwa pamoja” Richard Msimu.
Sambamba na kuchagua viongozi wapya Baraza hilo limepitia mapendekezo ya makisio ya Bajeti ya mwaka 2025/2026,Mwenyekiti wa Baraza hilo Seleman Pandawe amewasisitiza wafanyakazi wote kwenda kusimamia ukusanyaji wa mapato kidijitali ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa