KAMATI YA SIASA MKOA WA TABORA YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO-SIKONGE.
Kamati ya Siasa Mkoa wa Tabora imefanya ziara na kukagua miradi miwili ya maendeleo Wilayani Sikonge ikiwa ni miongoni mwa majukumu ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi.Dkt Batilda Buriani imekagua ukarabati na ujenzi wa baadhi ya majengo katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii(FDC) pamoja na Kiwanda cha kati cha kuchakata Mazao ya Nyuki.
Akisoma taarifa ya Ukarabati na Ujenzi wa majengo likiwemo bwalo la chakula,Mkuu wa Chuo hicho amesema mradi huo umegharimu Tsh.milioni 592.4 na kuongeza kuwa baada ya kukamilika kwake umesaidia kuongeza wanafunzi kutoka wanafunzi 92 hadi 217.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa Hassan Mwakasubi amewataka wasimamizi wa Miradi hiyo kuwa waaminifu ili kutimiza azma ya kuleta maendeleo kwa wananchi huku akiwashauri kuyatunza mazingira na miundombinu ili iweze kudumu kwa Muda mrefu.
Kwa Upande wake mjumbe wa kamati ya Siasa Maimuna Abasi amewashauri viongozi wa Chuo hicho kutoa elimu kwa wananchi hasa vijijini ili waweze kuja kupata elimu ya ufundi hatimaye wakajiajiri.
Katika mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki Mwenyekiti wa CCM Mkoa amewapongeza kwa hatua waliyofikia huku Mwenyekiti wa CCM mkoa amewataka viongozi na wasimamizi wa mradi huo kusimamia vyema vyama vya wafugaji wa nyuki ikiwemo kuwwpatia elimu ya ufugaji bora wa nyuki,kuwakopesha mizinga na kuhakikisha wanapata soko la uhakika katika kiwanda hicho ili waweze kunufaika na mradi huo.
Kiwanda hicho kinatarajia kutoa ajira za kudumu 22 kwa wananchi,na kuongeza kipato kwa wafugaji wa nyuki ambao watauza mazao ya nyuki katika kiwanda hicho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sikonge Anna Chambala ameiomba kamati hiyo kuwasaidia katika kuhakikisha wafugaji nyuki wanapata maeneo ambayo watafuga kutokana na changamoto ya baadhi ya wafugaji kupata vibali katika maeneo ya misitu.
Katika hatua nyingine Kamati ya siasa mkoa wa Tabora ambayo iliongozana na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo akiwemo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sikonge na wajumbe wengine wa kamati hiyo wameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kiwanda hicho cha kati cha uchakataji na usindikaji wa mazao ya nyuki.
Nae Kaimu Mkurugenzi Yusuph Hamza ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho na kuongeza kuwa kitasaidia kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi wa Sikonge na maeneo mengine pamoja na kuongeza pato la taifa na kuwa Kiwanda hicho kilicho katika hatua ya kukamilishwa kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani nane kwa siku na tani elfu mbili miamoja na nne kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa