MKUU WA MKOA AZINDUA BARAZA LA BIASHARA WILAYANI SIKONGE.
Na.Anna Kapama
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Buriani amezindua Baraza la Biashara la Wilaya ya Sikonge na kuzungumza na wadau na wafanya biashara .
Akitoa hotuba wakati wa uzinduzi Balozi Dkt. Batilda amesisitiza ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma ili kwa pamoja waweze kutekeleza malengo ya Baraza hilo,
Aidha Balozi Dkt.Batilda ameitaka Halmashauri kuingiza shughuli za baraza hilo katika bajeti ya Halmashauri pamoja na kuweka mpango mkakati kuendeleza viwanda,Biashara kupitia mpango mkakati wa Mkoa.
Sambamba na hilo Balozi Dkt.Batilda amesema muongozo wa uwekezaji wa Mkoa uchambuliwe ili kupata muongozo wa Wilaya na wananchi wajulishwe yanayotakiwa kufanyika kuinua uchumi huku akiongeza kuwa Baraza la biashara lifanyike Mara nne kwa mwaka likizingatia Sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa.
Akisoma taarifa ya baraza hilo Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sikonge Ndg.Selemani Pandawe,amesema madhumuni ya baraza hilo ni kuwa na jukwaa la majadiliano kati ya Sekta binafsi na Sekta ya Umma ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji sambamba na kupunguza gharama za biashara nchini ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Baraza hilo la wafanya biashara lenye wajumbe arobaini(40) kutoka Sekta binafsi na Sekta ya Umma linalenga kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji, kuibua fursa za uwekezaji na kuboresha utoaji huduma.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa